Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Mei 15, 2020

Ijumaa, Mei 15, 2020
Juma la 5 la Pasaka

Mdo 15: 22-31;
Zab 57: 8-12 (K. 10);
Yn 15: 12-17.

TUMECHAGULIWA KUWA WA MUNGU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kufurahia neema na baraka tulizoletewa kwa kipindi hiki cha Pasaka na neno la Mungu kwa karibu wiki sasa tumekutana na Yesu katika injili akiwapatia wale mitume wake wosia wa mwisho kabla ya ile siku ya mateso na kifo chake. Lakini wosia huu kwa kipindi hiki cha Pasaka basi tunautumia kama sehemu ya kutuandaa kwa sherehe ya kupaa kwa Bwana ambayo tutaifanya wiki ijayo. Katika injili yetu Yesu amekuwa akitupatia wosia muhimu tupaswao kuushika. Kuanzia jumapili iliyopita, Yesu alikuwa anasisitizia juu ya wanafunzi kubakia katika muungano naye na picha aliyotumia ni ya mzabibu na matawi katika kuelezea muungano huu. Sasa leo katika injili, wosia mwingine anaotuachia ni wa kupendana.

Anasisitiza kwamba upendo ni wa muhimu kwao kwani wao kama mitume wameitwa ili wakazae matunda-matunda yenye kudumu. Matunda wanayoalikwa kuyazaa ni kuwaongoa watu-kuwafanya watu wawe wafuasi. Sasa Yesu anawaambia kwamba bila kuwa na upendo, kamwe hawataweza kuzaa tunda lolote, hakuna atakayevutiwa nao hata ili ajiunge nao. Hivyo Yesu anasisitizia wapendane na anasema kwamba yeye amekwisha waonesha namna ya kupenda.

Ndugu zangu, tujiulize kwa nini upendo unakuwa wa muhimu kiasi hiki katika utume wa hawa mitume ili waweze kuzaa matunda mema? Hii ni kwa sababu kila mmoja, hata kama ni wanyama-kama paka, mbwa, ngombe-wote hawa wanatamani upendo na wakifahamu sehemu yenye upendo, hakika wanakaa karibu. Mfano, hata ukiwaangalia kuku, paka na mbwa-akikaribia yule anayewaonyeshaga upendo, unashangaa wanamfuata. Lakini akikaribia yule anayewanyanyasaga-wote humkimbia. Ndivyo ilivyo kwa wanadamu-wanadamu wanapenda sehemu yenye upendo. Hata watoto wadogo-licha ya udogo wao lakini siku zote utashangaa kuona kwamba hata katika kucheza kati yao na watoto wengine-hupendelea kufika zile familia zenye amani na upendo. Familia korofi huziepuka. Ndivyo ilivyo katika utume wowote wa kanisa ndugu zangu. Wanadamu tunatafuta upendo na wengi wakikutana na mtu aliyempenda, basi anakuwa tayari kumpatia moyo wake wote. Hata kama ni mke wako-mume unaweza kukuta haumjali halafu akikutana na mwanaume aliyemwonesha upendo hata wa juu juu tu, unashangaa anamuacha mume wake anakwenda kwa mwanamume mwingine kwasababu ya upendo.

Ndivyo ilivyo kwa utume wa kanisa. Watu wanatafuta upendo hivyo lazima jamii ya waamini iwe chanzo cha upendo ili watu waje, wapumzike, wafarijiwe, wapate kitulizo na kwa namna hii kweli kanisa linakuwa limezaa matunda.
Hivyo, kila mmoja wetu ajali upendo. Ajue kwamba kwa kuonesha ukatili, chuki, unawafanya watu wasimfikie Kristo. Hivyo, kila mkristo ajue ni wajibu wake kupenda ili azae matunda. Mume au mke tangaza upendo kwa mumeo na watoto. Usikubali akatafute upendo pengine na huko atakuwa tunda la shetani. Popote ulipo tangaza upendo, acha kuwatesa watu, ukikosa upendo unalikwaza kanisa.

Na hili suala la upendo ndilo hata tunaloliona katika somo la kwanza leo. Leo mitume wanaamua kwamba wale wakristo wasio Wayahudi sio lazima washike sheria za Kiyahudi. Kilichopo tu wajiepushe na mambo ya msingi kama uasherati, vyakula vitolewavyo kwa sanamu. Hili lilikuwa ni azimio lililoamuliwa na mitume kwa pamoja na ndani yake lilisheheni upendo na liliweza kulifanya lile kanisa la mwanzo liwe kama kitalu cha upendo. Liwe sehemu ambayo kila mmoja anakaribishwa; Wayahudi na watu wa mataifa-na huku ndiko kuzaa matunda ambako Yesu anakusema katika injili. Tafakari hii basi itufundishe tuone umuhimu wa upendo katika maisha yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni