Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Mei 14, 2020

Alhamisi, Mei 14, 2020
Juma la 5 la Pasaka

Mdo. 1:15-17, 20-26
Yn. 15:9-17

Ndugu wapendwa, leo tunaadhimisha sikukuu ya mtakatifu Matia Mtume. Habari zake na juu ya kuchaguliwa kwake kama mtume tunazisikia katika somo letu la kwanza leo. Yeye hakuchaguliwa na Yesu kama ilivyokuwa kwa akina Petro na wengineo lakini uchaguzi wake ulikuwa umeshatabiriwa kama tunavyoambiwa katika somo la kwanza kwani iliamriwa kwamba nafasi ya yule atakayeasi ichukuliwe na mwingine. Hivyo, utabiri huu ulitimia kwa Matia na hivyo Matia ni mtume halali ambaye uchaguzi wake ulitabiriwa kabla. Miongoni mwa sifa zilizomfanya achaguliwe ni pamoja na ukweli kwamba alikuwa shuhuda wa Yesu, aliona kila kitu tangu alipoanza utume wake kuanzia ubatizo wa yohane hadi kupaa. Aliona yote haya. Hivyo alimfahamu Yesu kikamilifu. Ingawa yeye hakuwa mtume, alijitahidi kuwa mfuasi hodari wa Yesu.

Tunachojifunza katika somo hili ni kwamba kazi yoyote tuifanyayo katika utumishi wa Bwana kamwe haitapotea. Utakuja kunieleza. Hata mimi mwenyewe naamini kuandika kwangu hizi tafakari sipotezi muda, ipo siku Mungu atailipa kazi yangu lakini kwa namna nyingine. Angalia Matia, yeye alijua kwamba hana hadhi kama ya akina Petro. Lakini hii haikumfanya yeye aache kumfuata Yesu. Alifuatana naye, akaona matukio yote aliyoyafanya, akatembea nyuma yake. Labda baadhi ya watu walimueleza kwamba unapoteza muda-weee! Mwisho wa siku akaja kuwa miongoni mwa mitume, miongoni mwa mababa wa kanisa, ambao kanisa limejengwa juu yao, na hawa ndio watakao uhukumu ulimwengu siku ya mwisho pamoja na Yesu. Kwa kweli ni bahati.

Hii ni changamoto kwetu na fundisho. Kamwe kama kuna wema wowote tunaoufanya, tuufanye kwa ajili ya Bwana, hata kama ni mgonjwa unatunza, au yatima unawapa chakula, au mtoto wa shule unasaidia, au unamzigo unajitwika kwa ajili ya wengine, au ni uongozi kanisani kama mwenyekiti jumuiya, katekista, wazee wa baraza-zote hizi hazina mshahara lakini nakueleza fanyeni kwa ajili ya Bwana. Nguvu zenu hazitapotea kamwe. Utashangaa kitu kimoja-baadhi ya wale walio viongozi kanisani au makatekista-ni watu wasiolipwa lakini utashangaa kuona kwamba familia zao siku zote zina hali nzuri-zaidi ya watu wenye mshahara. Najiulizaga je, inakuwaje? Naamini ni kwa sababu ya kazi wanazozifanya katika utumishi wa Bwana. Pia twajifunza baada ya kusali ni lazima tuende kutenda na kufanya kazi ili Mungu abariki mambo yetu. Baada ya kusali hawakusubiri tu Mungu achague bali walipiga kura, Mungu anatumia kipaji chako/nguvu yako kukuletea wokovu wako pia. Usisubiri tu usali bila kujishughulisha upate ulicho omba.

Pia wapo tuliopewa vipaji kwa ajili ya kanisa la Mungu. Usije ukadhani hata siku moja pengine kwa kuacha kwako kazi ya Mungu kama Yuda Iskariote Kanisa litaanguka. Watachagua mwingine tu kama Matia alivyochaguliwa na litasonga mbele hivyo usiligomee wala kuacha kujitoa.

Katika injili, Yesu tumesikia akiwaita wanafunzi wake rafiki. Kama rafiki alitegemea wasimuangushe, wawe wa kwanza kuupenda ule utume wake, wawapende na wale wafuasi wake pia. Nasi tutambue kwamba Yesu naye ametufanya kuwa rafiki kwake. Tutambue urafiki huu. Tuipende kazi yake ya kueneza injili, tusome maandiko matakatifu, tuyapeleke kwa wengine, tulipende na kanisa lake pia, tusikubali kuliona linaanguka na kuchekwa au kuacha kufanya kitu. Tuwapende na wale wenye uwezo wa chini na hali ngumu kimaisha, tusuwatenge na kuambatana na matajiri tu. Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni