Jumatano, Mei 13, 2020
Jumatano, Mei 13, 2020
Juma la 5 la Pasaka
Mdo. 15:1-6
Yn. 15 :1-8
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kufurahia neema na baraka tulizoletewa kwa sikukuu yetu hii ya pasaka na tafakari ya neno la Bwana leo tunaanza kwa kuiangalia injli yetu ambapo tunakutana na Yesu akiwaeleza wanafuzi wake maneno ya kutia moyo. Anawaambia kwamba yeye ni mzabibu nao ni matawi. Tawi hupata kila kitu toka kwa mti, tawi ni dhaifu na hivyo lazima linyenyekee kwa shina liweze kupata uhai. Hapa Yesu anatumia picha ya utegemezi-kati ya Yesu na wafuasi wake. Wao kama wafuasi ni lazima wapige hodi kwa Yesu kila siku na pale watakaposhindwa kufanya hivi, hakika watashindwa kuendelea mbele. Na hii kweli ilitokea: mara baada ya kifo cha Yesu, wanafunzi wengi walikosa Imani kwa Yesu na walijiona kudanganywa. Hivyo baadhi walitaka kurudia kazi zao za mwanzo na hivyo walikata tamaa sana; lakini Kristo alipokuja kwao na kuwavuvia Roho Mtakatifu, walipata kuanza upya na kuweza kuieneza injili sehemu nyingi na kuzaa matunda mengi sana.
Hapa twajifunza kwamba Yesu ndiye shina la wanafunzi hawa; pale waliposhindwa kumtegemea Yesu, wanafunzi hawa walishindwa kusonga mbele na kuzaa chochote. Sisi ndugu zangu kwa ubatizo wetu tunapata nafasi ya kujiunga katika shina yaani Yesu kama matawi. Hivyo, ubatizo hutuunganisha na shina hili na tukijua hili, tuzidi kubakia katika muungano na shina hili. Shina hili kwake tunapata sakramenti mbalimbali, tunapata neno linalotuletea matumaini na uhai. Tuepuke kujiunga kwenye mashina mengine; yapo mashina mengi-ya ulevi, ulafi, uchu wa mali, ubinafsi-tuyaepuke mashina haya. Sisi tujiunge kwenye shina la Yesu. Tujue kwamba mashina mengine yanatutaka tuyaendee lakini mwisho wa siku hatutafika popote-tunaweza kudhania kwamba tunafaidi lakini mwishowe hakuna faida yoyote. Mwishowe tutaangua kilio tu.
Somo la kwanza linatupatia habari za hali ya kutokuelewana iliyojitokeza katika Nyanja ya uijilishaji wa lile kanisa la mwanzo. Kulijitokeza makundi mawili-kundi la kwanza lilitoka kwa wakristo nao washike sheria za kiyahudi-kundi jingine halikuona haja ya kushika sheria hizi. Viongozi wa kanisa wanalitatua suala hili kwa hekima kubwa. Na mfumo walioutumia umekuwa ndio mfumo unaotumiwa na kanisa hadi siku hizi katika kuelezea na kutatua changamoto zake. Ni Roho Mtakatifu tu; ndiye aliyewawezesha hawa wakristo wa mwanzo kulitatua suala hili kwa amani hivi; bila Roho Mtakatifu, kanisa la mwanzo lingegawanyika makundi. Somo hili litufunze umuhimu wa Roho Mtakatifu aliyekuwa analiongoza kanisa katika utulivu mkubwa hivi. Tutambue kwamba Roho Mtakatifu hayupo katika fujo. Pale tuendekezapo fujo na maslahi binafsi mbele na kusahau kumwomba Rkho Mtakatifu aliongoze kanisa letu, mambo huharibika tu. Tondoe suala la maslahi. Jumuiya nyingi za kikristo zinavunjika kwa sababu ya viongozi kutanguliza maslahi mbele. Tuondoe maslahi katika kazi ya Mungu. Mitume waliamua kwenda Yerusalemu kulitatua hili kwa sababu hawakuwa na maslahi binafsi. Nasi pia tutambue umuhimu wa masikilizano ma majadiliano katika kulijenga kanisa letu. Usikubali kuamua kila kitu mwenyewe tena pengine kwa kufuata vionjo vyenye maslahi binafsi hata kama wewe ni Paroko, au mkuu fulani, Kiongozi yeyote, jadilianeni kwa kusikilizana na hili huacha mioyo ya wote katika amani na hapo wote hujitoa kwa moyo kulitumikia kanisa zaidi na kubaki ndani ya mzabibu mmoja. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni