Jumatatu, Mei 11, 2020
Jumatatu, Mei 11 2020.
Juma la 5 la Pasaka
Mdo 14:5-18;
Zab 115:1-4,15-16 (K. 1);
Yn 14:21-26.
MUNGU ANAISHI NDANI MWETU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kufurahia neema na baraka tulizoletewa kwa sikukuu yetu ya Kristo mfufuka na tafakari ya neno la Bwana leo linaanza kwa kuiangalia injili yetu hapa Yesu anatupatia maneno matamu kabisa: anasema kila ampendaye atazishika amri zake na Baba atampenda halafu Yeye na Baba watakuja kwa huyu mtu. Na hii huwa faida kubwa kwa huyu mtu kwani maisha ya mkristo, juhudi zote anazozifanya lengo lake ni ili Baba na Yesu aje na kukaa ndani yake. Tunapokea sakrament zote hizi, tunakazana kuishi maisha ya kimaadili, tunakazana kusoma Biblia, wengine tunasoma theologia na philosophia; tunahudhuria misa kila siku kwa wengine na wengine tunakuja jumuiya na kujiunga na vyama mbalimbali vya kitume au hata kwenda kutoa misaada mbalimbali kwa watu lengo likiwa ni ili Yesu na Baba waje na kukaa ndani yetu. Haya ndiyo mafanikio makubwa kwa mkristo-kuweza kumshawishi Yesu na Baba waje na kukaa ndani yake. Hili likishatokea mkristo sasa anaweza kutulia, anaweza kuungana na Simeoni katika injili ya Luka na kusema “sasa Bwana wamruhusu mtumishi wako aende kwa amani” hapa mkristo anaweza kuungana na mtakatifu Paulo na kusema “mimi sitajivunia chochote isipokuwa msalaba wa Yesu Kristo.” Hii ni hali ya uhusiano mkubwa sana na Mungu na watakatifu kama akina Mtakatifu Paulo na Francisko na watakatifu wengine wengi waliweza kufikia hatua hii. Ni Kristo aliyekuja na kuishi ndani na kuwawezesha kuweza kuishi ufukara wa hali ya juu kabisa, wakaweza kukaa muda mrefu katika sala na tafakari, wakaweza kufanya matendo ya huruma kama akina Mtakatifu mama Teresa-wewe unafikiri kwamba Mama Teresa angeweza kufanya matendo ya huruma mengi hivyo bila nguvu ya Baba ndani yake? Labda tujiulize: kuna wenye pesa wengi. Nao pia wanafanyaga matendo ya huruma? Sasa niambie, (weka yeyote unayejua ni tajiri)- ni tajiri sana kuliko alivyokuwa mama Teresa au mtakatifu Francisko. Lakini kwa taarifa ni kwamba huyo hajaweza kufanya hata nusu ya kile alichofanya mama Teresa au mtakatifu Francisko au mtakatifu Paulo. Niambieni ni kwa nini. Siandiki ili kumdharau tajifi huyo lakini lengo langu ni kuonesha kwamba Yesu na Baba walikuwa ndani ya mama Teresa na ndio maana aliweza kufanya hivyo na endapo kama Yesu na Baba watakuja na kukaa ndani yake, naamini nao watafanya makubwa.
Ndugu zangu, kwa mifano hii naomba tujifunze faida za Yesu na Baba kukaa ndani ya maisha ya mkristo. Hii ndilo tamanio kuu kuliko lolote kwa maisha ya Mkristo. Na pale tutakapofaulu kumleta Yesu na Baba ndani yetu, basi tuwe makini: utukufu wote na sifa yote tutakayopata tumrudishie Baba kama mtakatifu Paulo na Barnaba wanavyofanya katika somo la kwanza. Walijua kwamba ni Roho wa Baba aliyewawezesha kufanya miujiza yote mikubwa na hivyo wakawa tayari kumrudishia Baba utukufu wake. Nasi tujue kwamba Baba lazima tumpatie utukufu wake. lakini tutambue kwamba sisi kama wakristo tutaweza kufanya mengi kama tutamruhusu Yesu na Baba kukaa ndani yetu. Tuwapatie nafasi waje kwetu. Na sisi wenye kauwezo kadogo na ambao labda tunajitahidigi kufanya matendo ya huruma, tutambue kwamba tutaweza kufanya mengi endapo Yesu na Baba watakuwa ndani yetu. Hivyo, kabla ya kufanya matendo ya huruma, tusali kwanza kumwomba Baba Baraka na hakika tutaweza kufanya mengi zaidi. Naona bado tunachokifanya ni kidogo bado. Tukazane, tusali na kweli tutaweza kufanya makubwa Zaidi. Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni