Jumamosi, Mei 09, 2020
Jumamosi, Mei 9, 2020
Juma la 4 la Pasaka
Mdo 13:44-52;
Zab 98:1-4 (R. 3);
Yn 14:7-14.
MUNGU KUDHIHIRIKA NDANI YA MAISHA YETU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kufurahia neema na baraka zilizoletwa na ufufuko wa Kristo na neno la Bwana leo tukianza kwa kuiangalia injili, tunakutana na Yesu akiongea na Philipo kwa msisitizo mkubwa. Philipo anaonesha hali ya kukosa imani kwa Yesu, amekaa na Yesu siku zote na anashindwa kuona upekee wowote ndani ya Yesu: yeye anamuona tu kama mtu wa kawaida, hajaweza kuona muunganiko na uhusiano kati yake yeye na Baba tangu alipoweza kumfufua Lazaro kutoka wafu, tangu alivyoweza kuwalisha wale makutano na katika miujiza yote aliyokuwa anafanya Yesu. Philipo kashindwa kuona chochote kile ndani ya Yesu, na mbaya Zaidi ni kwamba Philipo katika injili ya leo anaonekana kutokutosheka na kile ambacho Yesu amekwishafanya; yeye anataka Zaidi, anataka aoneshwe Baba na ndipo atosheke, Yesu bado hajamtosha. Yesu anashtuka na anaamua kumjibu Philipo tena kwa ukali kwa kumwambia kwamba imekuwaje ati yeye ameshindwa kuona upekee wowote ndani ya Yesu, inakuwaje ati ameshindwa kuona uhusiano uliopo kati yake yeye na Baba; Yesu ni kama vile anamwambia Philipo kwamba unafikiri hii miujiza yote iliyokuwa inafanyika, kufufua watu kote kulikofanyika unafikiri kulitokea kibahati bahati? Hukuweza kuona muunganiko wa Baba na Mimi? Hukuweza kuona ndani yangu njia ikupelekayo kwa Baba? Hivi ndivyo Yesu anavyomweleza Philipo kwa msisitizo mkubwa.
Ndugu zangu, hali ile ya Philipo kumzoea zoea Yesu, ile ya kukaa naye, kula naye, kuongea naye ilimfanya ashindwe kuona chochote cha ziada ndani ya Yesu. Hali hii ilimfanya amwone Yesu kama rafiki tu wa kawaida, kama mwanadamu mwenzao, kama mwanamazingaumbwe tu wa kawaida waliokuwa wanaishi kwa wakati ule. Hali iliyomkuta Philipo inaweza kutukuta na sisi hasa pale tuzichukuliapo Sakramenti kama kwa kimazoea. Mkristo anapozizoea sana Sakramenti-mwishowe hushindwa kuona utakatifu uliopo ndani ya hizo Sakramenti na mwishowe huishia kuziona kama vitu tu vya kawaida vile kama Philipo alivyomzoea Yesu na kuishia kumwona kama wa kawaida tu usiyeweza kumwona Baba ndani yake. Sisi tuziheshimu vyema sakramenti zetu hasa sakramenti ya Ekaristi. Tuipokee kwa Imani. Tujue kwamba sakramenti hazizoeleki. Siku zote ni takatifu. Hata Misa Takatifu haizoeleki. Siku zote hubakia katika utakatifu ule ule. Tuache kuzoea mambo matakatifu.
Sakramenti nyingine ambayo watu tunaonesha mazoea mabaya nayo ni sakramenti ya ndoa.
Ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu watu tumeizoea mno hii sakramenti na kushindwa kuona utakatifu unaopatika ndani ya sakrmenti hii. Watu hawaoni umuhimu wa kufunga ndoa. Wanaona ni afadhali kufika hata miaka sitini bila ndoa. Hawajui kwamba sakramenti ya ndoa hutoa neema ya kuwawezesha wanandoa kuishi pamoja. Hii hawaikubali.-na kati ya maeneo ambayo kwa kweli kanisa tunahitaji kukazania ni hapa. Kwa mtazamo wangu, nafikiri Zaidi ya nusu ya waamini, hasa sisi tulio vijana-hatujui kwamba ndani ya sakrament ya ndoa kunapatikana neema; yaani sakramenti ya ndoa hutoa neema inayowapatia wanandoa nguvu ya kuungana pamoja. Hii hatujui na kwa kweli jamani tuongeze bidi hapa hasa katika kuinjilisha.
Katika somo la kwanza, tumesikia mtume Paulo na Barnaba wakihubiri injili kwa Wayahudi lakini Wayahudi nao wanaikataa; wanajivuna na kufikiri kwamba wao walikwisha kuchaguliwa na Mungu na hivyo hawaoni chochote kipya ndani ya kile wanachohubiri akina Paulo. Paulo anawaeleza kwamba wawe makini kwani watakuja kushangaa kwamba watu wa mataifa wanafaidi na wao wanadidimia. Hii ilitokea kwani watu wa mataifa walikuja kuwapita Wayahudi hasa katika Nyanja ya Imani. sisi ndugu zangu tujue kwamba Imani yetu inahitaji kufanywa upya (updates) kila siku. Hata kama wewe ni mtawa au karesmatiki au nani. Jua kwamba Imani haizoeleki, unahitaji kujitahidi kila siku, kuomba Mungu, maisha ya Imani ni mapambano. Hivyo lazima upambane. Usijitangaze mtakatifu ukiwa duniani. Pia usikubali kutangazwa mtakatifu ukiwa bado duniani; usibetweke na na sifa za wenzako. Twahitaji kupambana hadi mwisho. Tusizoee sala zetu na kusali bila kufikiri unasema nini, utazichoka na badae utatunga zakwako na hata za kwako utazichoka, na mwishowe utahama makanisa kila siku na hata hizo za makanisa mengine utazichoka tena na utaishia kuzurura hata kifo kinaweza kukuta hujafanya kitu. Sala inapaswa kuwa mpya siku zote. Ndani ya "Baba yetu" hiyo hiyo utapata neema tele, ndani ya "Salamu Maria" hii hii unapata neema tele. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni