Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Mei 08, 2020

Ijumaa, Mei 8, 2020,
Juma la 4 la Pasaka

Mdo 13: 26-33;
Zab 2: 6-11;
Yn 14: 1-6.

MBINGUNI NI NYUMBANI KWETU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Bado tunaendelea kufurahia neema na baraka tulizoletewa kwa sikukuu yetu hii ya Paska na neno la Bwana leo katika somo la Injili tunakutana na sehemu ya wosia wa mwisho wa Yesu kabla ya kifo chake na anawaambia wanafunzi wake maneno ya matumaini kwamba nyumbani mwa Baba mna makao mengi na yeye anapoondoka kwao ni kwamba anakwenda kuwaandalia makao hayo. Na anazidi kusisitizia juu ya hili kwa kumwambia Philip kwamba yeye ndiye njia ya kwenda huko. Hivyo, wakibakia katika kumtambua na kumwamini Yesu hakika hatawaacha bali atakuja kuwapeleka pale yeye alipo. Hii ilikuwa ni habari njema sana na Yesu alitaka wote waifahamu, yaani wote waambiwe habari hizi ili wamwamini Yesu na Yesu apate kuwapeleka pale alipo katika makao ya Baba. Na mitume walikazana kuhakikisha kwamba watu wote wanapata kujua habari za Yesu haraka iwezekanavyo ili nao wapate kuwako pale Yesu alipo.

Katika somo la kwanza tunakutana na Mtume Paulo akikazana kumhubiri Yesu mfufuka na anawataka watu waongoke na kumwamini huyu Yesu mfufuka ili nao wapate kupelekwa pale Yesu alipo. Katika kuifanya kazi hii, Mtakatifu Paulo alikumbana na adha nyingi, alipigwa mawe, akachapwa viboko na hata kuvunjikiwa na meli baharini na hata kunyeshewa mvua lakini mwisho wa siku bado alizidi kuihubiri hii habari njema akitaka watu wamwamini Yesu na kupelekwa pale alipo Yesu.

Ndugu zangu, huu ujumbe wa neno la Mungu leo ni wa muhimu sana kwetu. Wengi tunahitaji tutiwe moyo na ujumbe wa namna hii kwani kwa kweli duniani tunapataga mahangaiko. Fikiria unakuta mzazi labda kakazana kazaa watoto wake, kawalea, kawasomesha na labda kauza hata mashamba yake yote amsomeshe mtoto. Lakini mtoto mwishowe anafeli shuleni na kushidwa kufanikiwa hivyo inakubidi wewe mzazi uteseke hadi uzee wako-unakuta wazazi wanafanya kazi za vibarua au kulinda usiku kwa sababu watoto wanamtegemea na alitoa mali zake zote kuwasaidia hawakufanikiwa. Hivyo, hadi uzee unateseka. Jamani. Haya maneno ya Yesu kwamba kwa Baba kuna makao ndio yatakayompatia moyo wa kusonga mbele mzazi aliyekumbwa na shida za namna hii. Bila maneno ya namna hii aweza kukata tamaa. Au kingine unakuta mzazi kajitahidi kutoa karibu kila kitu kuwaendeleza watoto wake na wale watoto wanafanikiwa na mwishowe hawamkumbuki. Unakuta mzazi yuko kijijini anasukuma mkokoteni hadi uzee jamani na watoto aliojihangaisha nao hawamjali. Bila maneno ya matumaini na ya Imani kama yanayotolewa katika injili ya leo, mzazi wa namna hii aweza kukata tamaa ya maisha. Au labda mtu ndio umekazana kubana fedha zako na kujenga jengo lako la kitega uchumi, ukakodisha watu pale ili watu wafanye biashara na wewe ukusanye kodi ikusaidie katika uzee wako na gafla inatokea bomoa bomoa inaangusha jengo lote-nakwamba kama huna Imani waweza kukata tamaa vibaya sana.

Kwa kweli duniani kuna shida: kuna kina Mama ambao watoto wao ni wagonjwa; yaani mtoto uliyemzaa ukitegemea kwamba atakukomboa bado anazidi kukudai hadi senti ya mwisho. Yaani badala ya kuzaa msaada unazaa msalaba wa kukusumbua maishani mwote. Zote hizi ni shida na kwa maisha ya wanadamu. Lakini kwangu mimi binafsi kama mkristo huwa nikikutana na maneno haya ya Yesu kwa wanafunzi wake kwamba anakwenda kuwaandalia makao na yeye ndiye njia huwa ninatiwa moyo sana. Hata hizi shida za ulimwengu kama vile za kutokupokea msaada kwa mtu ambaye labda hapo mwanzo nilimwandaa aje akanitunze-huwa nikikutana na maneno haya ya Yesu huwa nafarijika sana. Ebu jamani tutulie na kuvuta pumzi kidogo na kuona utamu wa haya maneno. Nakwambia haya maneno kwangu hata kama nina shida kiasi gani nikishakutana nayo huwa zinatulia na wakati wa shida na msongo wa mawazo hii sehemu ya injili ndio nakujaga kusoma. Ni maneno matamu sana. Basi maneno haya yatutie moyo hasa sisi ambao kila kukicha tunahangaika lakini mwisho wa siku kile ulichokihangaikia tangu asubuhi unakuta hakija kuletea faida yoyote. Pia yawatie moyo wale wanaowatumikia wagonjwa mbalimbali na waliopitiwa na bomoa bomoa. Pia sisi tuwe watu wa kuwatia moyo wenzetu hasa wale walio katika kukata tamaa kabisa. Tumisfu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni