Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Mei 05, 2020

Jumanne, Mei 5, 2020
Juma la 4 la Pasaka.

Mdo 11:19-26;
Zab 87:1-7 (K. 117:1);
Yn 10:22-30.

IMANI NI LUGHA YA KUMFAHAMU MUNGU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Kama kawaida bado tunaendelea kufurahia neema na baraka tulizoletewa na Mwenyezi Mungu kwa kipindi hiki cha Pasaka. Na neno la Mungu leo katika injili bado linaendelea kutukumbusha juu ya Yesu kama mchungaji mwema na kama mchungaji mwema, anakuwa mkali kwa wale wanao mchezea akili, hawa ni baadhi ya viongozi wa Kiyahudi. Leo wanamfuata na kumwambia kwamba ati kama yeye ni Masiha, awaambie tu. Yesu anakasirika kwani hawa ni watu wanaokuja kwake si kwa lengo la kumwamini lakini kwa lengo la kutafuta mada ya kuwa chanzo cha yeye kugombana nao. Na Yesu anawaambia ukweli kwamba wanadiriki kufanya yote haya kwa sababu wao sio kondoo wake, wangekuwa kondoo wake, ungekuta tayari wamekwisha mwamini, wamekwisha sikia sauti yake na kumfuata. Wasingekuwa wanamzungusha zungusha kwa kuja na kumwambia ati kama wewe ni Masiha tuambie; hapa walikuwa wanamchokoza tu. Kama kweli walitaka kumwamini, wasingekuwa na haja ya kumwuliza swali hili. Wangekuwa wamekwishamwamini tayari. Ndugu zangu, hawa viongozi walikuwa na lengo la kumpima Yesu na lengo lilikuwa Yesu atoe majibu ambayo labda yangepingana na mafundisho ya dini yao ili labda akosane na watu, ili Yesu asipate tena wafuasi. Na kwa kweli huku siko kuwa kondoo wa Yesu. Hii tabia walikuwa nayo sana.

Ndugu zangu, sisi tunapaswa kuepuka tabia kama hizi. Wapo baadhi yetu tulio na tabia za kuwategea watu, mtu unajua kwamba huyu ana udhaifu huu. Hivyo, unamjengea mazingira ambayo labda yatamfanya aseme au atende kitu fulani ili aanguke. Hata katika ndoa; ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya kutegeana. Unakuta mmoja anafahamu udhaifu wa mwenzake lakini hatamuonea huruma na kumsaidia, atamtegea tu, atamtafutia mtego tu na hii inasababisha kuvunjika kwa ndoa. Jamani hii sio tabia za kiukarimu. Lazima tuwe wakarimu kwa wenzetu. Usimtegee mwenzako alafu akisha anguka unaanza kushangilia.

Katika somo la kwanza tunazidi kuona jinsi habari za Kristo mfufuka zinazidi kuenea sehemu na mipaka mbalimbali. Kwa kweli tunaweza kuona jinsi Wakristo wa mwanzo wanavyojitolea kwa ajili ya injili. Pia walionesha ushirikiano mkubwa kati ya wao kwa wao na waliweza kufika mbali. Walisaidiana katika udhaifu na leo kwa mara ya kwanza, baada ya watu kuwaona jinsi walivyoungana na wanavyofanya kazi zao, wale watu wanawaita kwamba wao ni Wakristo-yaani wao ni kitu kimoja, wenye nia moja, na kiongozi wao ni Kristo. Jambo hili lilikuwa sehemu ya mafanikio makubwa sana kwa hili kanisa la mwanzo. Kweli wamemuishi Kristo na hivyo wamepatwa kuitwa wakristo. Hilo jina likawa ndio nembo ya dini yetu hadi leo. Lakini tunajiuliza, je, kweli tunastahili kuitwa Wakristo kama wale wazee wetu wa mwanzo kule Antiokia? Wao walipewa hili jina na watu na sio kwamba walilikuta na kulirithi. Wangekuwa watu wanaotegeana ua kukwaza wasingeitwa jina hili la Wakristo. Wangeitwa jina jingine. Ndugu yangu, unachokifanya na kukithamini ndicho kitakachokupa jina. Wewe jiulize, nini kinachokupa jina? Tukijiunga na kufanya yale ya Kristo, watu atamuona Kristo ndani yetu. Tusafishe majina yetu leo Kwa kujiunga na Kristo zaidi.

Maoni


Ingia utoe maoni