Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Mei 04, 2020

Jumatatu, Mei,4 2020.
Juma la 4 la Pasaka

Mdo 11:1-18;
Zab 42:2-3,43:3-4 (K. 42:3);
Yn 10:11-18.

KUMFUATA MCHUNGAJI MWEMA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo, bado tunaendelea kufurahia na kumshukuru Mungu kwa neema na baraka alizotujalia kwa kipindi hiki cha pasaka na neno la Bwana tutaanza kwa kuliangalia somo la injili ambapo tunakutana na Yesu akituendelezea ile maada ya jana kwamba yeye ni mchungaji mwema. Yesu ameamua kuwa mchungaji mwenyewe kwa sababu ya wale waliokabidhiwa kazi hii katika taifa la Israeli waliishia kuwapotosha kondoo. Hawa walikuwa ni Wafalme, Makuhani na viongozi wengine wa dini na serikali katika taifa la Israeli. Waliambiwa wawalinde kondoo, wawaongoze katika kumjua Mungu, watumie rasilimali zilizopo kuwalisha wale kondoo waliokabidhiwa. Lakini wao waligeuka na kuona nafasi waliyoipewa kama sehemu ya kuanza kujinufaisha na kuwaacha kondoo bila mchungaji. Mwishowe watu hawa waliishia kupotoka na kufa kutokana na ukosefu wa mwongozo wa neno la Mungu, kukosa mifano mizuri katika maisha na kupatiwa mifano mibaya ya maisha na kukosa mtu aliyewalisha katika malisho salama. Hata wakaenda utumwani tena.

Sasa Yesu ameamua kuchukua kazi hii ya mchungaji yeye mwenyewe. Lakini anapochukua kazi hii, ugumu anaokumbana nao ni wa kuwapata kondoo. Mwanzoni kondoo walikosa mtu wa kuwaongoza lakini sasa wamepata mtu lakini wanakataa kumfuata. Lakini Yesu anazidi kuwasisitizia kwamba yeye ni mchungaji mwema na anawaambia wamfuate. Yesu hachoki kuwaita na kuwapatia mfano wa maisha-japokuwa wachache ndio wanaomkimbilia.
Injili hii yatufundisha mengi ndugu zangu. Inatualika nasi tuwe wachungaji wema. Kila mmoja ajue kwamba kakabidhiwa kakundi chake. Hivyo, unapoonesha mfano mbaya, hata kama wewe sio Padre au Mtawa au Mzazi jua kwamba kuna anayekwazika, au kujifunza mfano mbaya unapofanya vibaya. Watoto wengi wamejifunza maadili mabaya toka kwa watu ndani ya jamii inayowazunguka. Hivyo, tuepuke kuonesha mfano mbaya hata ndani ya jamii tusiyofahamika. Wengi wetu kama tunataka kutenda uovu wetu huwa tunatabia ya kwenda mbali kabisa, sehemu tusiyofahamika na yeyote ili tutende uovu wetu. Lakini nakwambia tambua kwamba ukiwa huko ndiko unawakwaza watu Zaidi-kwani ukiwa kule wale vijana au watoto wanaokuona kule hawajui cha kwamba umetokea wapi wao wanachohusika nacho ni kile wanachokiona ukitenda. Hivyo tutambue kwamba wale tunaokwendaga kufanyia uovu wetu kwenye maeneo ya mbali, tujue hapa tunakwaza Zaidi na kuwapotosha wengi. Tabia hii tuache. Tuwe wachungaji wema.

Katika somo la kwanza tumesikia jinsi Petro alivyokumbatia agizo la kuwa mchungaji mwema na kwa uchungaji wake ameweza kuipeleka injili hata kwa watu wa mataifa mengine na anakuwa tayari kujitetea mbele ya chama cha wafarisayo kwamba alichofanya ni chema. Nasi ndugu zangu tujue kwamba tunalojukumu la kuwatetea kondoo wetu hasa pale wanaposhambuliwa na watu wasiowafahamu. Wale wakristo toka katika kikundi cha wafarisayo walimuona Petro kama mdhambi na asiyeshika sheria kwa kitendo chake cha kuipeleka injili kwa watu wa mataifa mengine. Lakini yeye aliweza kuwatetea na polepole wale wakristo waliokuwa wanatokea katika kile kikundi cha wafarisayo walimuelewa. Nasi tujue kwamba tunalojukumu la kuwatetea wenzetu hasa wale wanaodhaniwa au kufikiriwa vibaya. Kuna wenzetu ambao bado wanaonekana kuwa ni wabaya lakini kwa undani ni kwamba ni baadhi ya watu wamekataa kuwaelewa. Sisi tujue kwamba jukumu letu ni kuwatetea na kuwafanya waeleweke na watu. Kuna watu wanachukiwa lakini kiundani ni kwamba ni jamii tu imeshindwa kuwaelewa. Hivyo tuwe tayari kuungana nao ili wasiendelee kukandamizwa na jamii. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni