Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Mei 02, 2020

Jumamosi, Mei 2, 2020
Juma la 3 la Pasaka

Mdo 9: 31-42;
Zab 116: 12-17;
Yn 6: 60-69.

UNA MANENO YA UZIMA WA MILELE!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kufurahia furaha tulizoletewa na sikukuu yetu ya Pasaka na neno la Bwana leo katika injili Yesu anaendelea kufundisha juu ya yeye kama mwili ambao utabidi uliwe na yeyote atakayeula hakika atapatiwa uzima wa milele. Fundisho hili linakuwa gumu kupokelewa hata na baadhi ya wanafunzi wake na Yesu anapoona kwamba hata wanafunzi wake wanapatwa na kigugumizi katika kulipokea hili, yeye mwenyewe anashtuka. Alitegemea kwamba wale wanafunzi ndio wawe mstari wa mwanzo katika kumsaidia lieleweke. Lakini cha ajabu ni kwamba wao wanajiunga tena na lile kundi la wale Wayahudi, wale waliokataa kulipokea fundisho hili. Ndugu zangu, wanafunzi wa Yesu hawakuwa na sababu ya kukataa kulielewa fundisho hili. Wao wangalipaswa kulipokea, wao wangetakiwa mpaka sasa wawe wamekwisha mwelewa Yesu kwamba huwa hadanganyi na kila asemacho ni ukweli. Kitendo cha kukataa kulipokea fundisho ni dhahiri kwamba walikuwa bado hawajamwelewa vizuri na hivyo walikuwa bado wanamtilia yYsu shaka. Hivyo, wao wangalipaswa kulipokea neno hili ili watu wengine wapate moyo kulielewa. Yesu aliwategemea sana wafanye hili.

Nasi ndugu zangu inatupasa kutambua kwamba Yesu naye anatutegemea sana. Anategemea sisi tumuamini na kuamini mafundisho yake ili yaweze kuwafikia wengine kirahisi. Usipoamini wewe, ambaye ni Mkristo, wewe ambaye Yesu anakutegemea, mimi padre ambaye Yesu ananitegemea, mimi mzazi ambaye watoto wananitazama, je, wengine wataamini vipi? Yesu anatutegemea, tusimwangushe. Tutambue kwamba kutokuamini kwetu, kukufuru mambo matakatifu na kulisema kanisa vibaya kunawakwaza wengi wasimwamini Yesu. Hivyo jamani tumtetee huyu Yesu wetu, anatutegemea, tusimwangushe. Kama wewe utamwangusha, je, wengine wataamini vipi? Wewe ambaye umeishi na Yesu sasa na una miaka mingi sasa katika imani, oneshe kwa matendo kwamba sasa unamuelewa Yesu, kwani Yesu anakutegemea usijiunge nawasio lipenda kanisa na kuanza kulishambulia, linda imani yako.

Katika somo la kwanza, tunaikuta imani ya Kristo mfufuka ikiendelea kupelekwa na kuhubiriwa mbali Zaidi na Zaidi. Jana Yesu mfufuka alimgeuza mtesi wa kanisa kuwa mtume wake (Paulo). Leo nguvu ya Yesu inatenda muujiza wa kumfufua mtu kutoka wafu. Lengo ni kutufanya tuiamini habari njema ya Kristo mfufuka iliyofika kwetu na kwa kuamini kwetu tupate uzima. Nasi kwa siku ya leo tumwombe Kristo asituache, apite kwetu, atutendee na sisi muujiza na atuletee amani kama alivyoleta Amani kwa familia hii ya Dorcas iliyokuwa katika maombolezo makali. Atufufue kutoka katika dhambi zetu zinazo tufanya tuwe wafu wa kiroho. Fikiria juu ya dhambi inayokutesa kila wakati na unairudiarudia daima, pengine ni majivuno, kukosa unyenyekevu, kupenda sifa kupita kiasi na kuzitafuta huku ukiwaonea wadogo, kupamba watu kwa maneno ya uongo badala ya kuwaambia Ukweli? n.k. Mwewe akitaka kumuua nyoka humbeba juu kwani anajua lazima abadilishe uwanja Wa mapambano kwani akiwa chini anajua hatamweza nyoka, hata sisi lazima tubadilishe mazingira ambayo tunajua shetani anatukamata kirahisi- badilisha uwanja wa mapambano- kama wewe unajijua una shida ya ulevi na unataka kuacha kwanini ukakae baa? Yapo mazingira/watu wanautufanya tutende dhambi lazima tubadili uwanja wa mapambano kwa nguvu ya Yesu mfufuka, tuwe viumbe vipya. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni