Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Mei 01, 2020

Ijumaa , Mei 1, 2020.
Juma la 5 Pasaka

Kumbukumbu ya Mt. Yosefu Mfanyakazi

Mdo 14: 19-28;
Zab 145: 10-13, 21 (K. 12);
Yn 14: 27-31.

Au masomo ya kumbukumbu

Mwa 1:26-2:3; au Kol 3:14-15, 17, 23-24
Zab 90:2-4, 12-14, 16 (K. 17);
Mt 13:54-58.

MT. YOSEFU MFANO WA WAFANYA KAZI

AMANI YA KRISTO INAYO FARIJI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo kwa namna ya pekee tunaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu mfanyakazi. Huyu alikuwa mfano wa Baba bora wa familia yake. Alikuwa Baba wa kawaida, aliyepata mahitaji yake kwa kufanya kazi; kazi yake ilikuwa ya useremala kama injili ya leo inavyotuambia na inaonekana kwamba kazi hii ilimfanya afahamike kijiji kizima na waliitumia kama kitambulisho chake. Na kwa kweli hii ilikuwa ni sifa kubwa kwa Yosefu: ametambulishwa kwa ile kazi aliyokuwa anafanya-ya useremala. Kwa mazingira ya kijamii, mtu kukutambulisha kwa kutumia kazi yako ina maanisha kwamba kwa kweli huyu ni mtu aliyekuwa msaada mkubwa kwa ile jamii-aliweza kuwafanyia kazi zao nyingi na watu wengi walikuwa wamezoeana naye.

Halafu kingine, ni kwamba kitendo cha watu kumtaja Yosefu kama seremala inaonekana kwamba pale kijijini alikuwa mtu wa kawaida sana-alikuwa na uwezo wa kawaida kifedha kwani endapo angekuwa na uwezo mkubwa Zaidi-basi hawa watu wa kijijini mwake wangetafuta njia nyingine ya kumtambulisha Yosefu. Wasinge mtambulisha kirahisi rahisi hivyo. Yosefu alikuwa mtu wa watu, aliyeweza kufikiwa na kila mtu, aliyewafanyia watu kazi zao kiasi cha kutumia kazi yake kama kitambulisho chake. Huyu ndiye Yosefu.
Kwa kazi hii, yeye aliweza kuilisha familia yake; alimtunza Yesu, haisikiki mahali popote kwamba Yesu aliwahi kushikwa na utapiamlo au kutelekezwa mtaani. Haikusikika popote kwamba Yosefu alimtelekeza Mama Maria. Yeye alibaki pamoja naye kwa kipindi chote cha shida tangu kukimbilia Misri ili kumwokoa mtoto. Hii ni tofauti kabisa na baadhi ya wababa wa siku hizi: baadhi hutoroka nyumbani ifikapo mwisho wa mwezi wakikimbia makusanyo ya kodi za nyumba; huwaachia mzigo akina mama; mzigo wa kugombezwa. Wengine wakikopa mikopo-ifikapo muda wa kulipa, hutoroka na kuiacha familia katika mateso. Wengine huenda kujirusha na kula starehe wakiiacha familia bila chakula, wao wanashiba kitimoto huko njee, wakati watoto wanapiga miayo nyumbani, wao wanazunguka kwenye viti virefu wakipata kinywaji baa wakati mama anazunguka shambani kutafuta matembele angalao kupooza njaa. Yosefu anafaa kuwa mwombezi na kiongozi kwa akina baba kama hawa-wanaokataa kutimiza majukumu yao.

Katika somo la kwanza, tunasikia habari za uumbaji na jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na kumkabidhi dunia iliyosafi impatie riziki yake na kumtunza. Tunapaswa kuitumia vyema, itutunze, tusichafue mazingira yake. Pia tunaaliwa kushirikishana rasilimali za hii dunia. Hii dunia ni ya Mungu, lakini kuna walio binafsisha sehemu za hii dunia na kuwazuia wengine wasizifikie. Sehemu hizi zina ardhi safi, maji na madini. Hawa wanazitumia wenyewe na kuwaacha wengine wakiwa katika ardhi ya jangwa, ukame na isiyo na rasilimali yeyote. Ni jukumu la wale walio katika sehemu zile zenye rasilimali nzuri kushirikishana na wenzao. Jamani nchi imejaa fadhili za Bwana. Tushirikishane hizi fadhili za Bwana. Watu wanakufa njaa kwa sababu hawashirikishwi hizi fadhili za Bwana tulizopewa hapa duniani. Wengine wamezichukua, wakatia uzio na kufuli na kuziacha zioze wakati wengine wanakufa njaa. Tupingane na ubinafsi huu. Kingine ni kwamba lazima tuitunze hii dunia tuliyopewa hata wale wa vizazi vijavyo nao waifurahie. Tusiwe wabinafsi kiasi cha kuvisahau vizazi vijavyo. Tuache uchafuzi wa mazingira. Mungu atusaidie sote. Wale mnaotesa wafanyakazi acheni-mwogopeni Mungu, mnaotoa mshahara kidogo wa kionyonyaji badilikeni;shirikishana fadhili za Mungu na wafanyakazi wako. Acheni uroho, na ulimbikizaji wa mali vyote nivya Bwana utaviacha kama ulivyovikuta.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni