Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Aprili 29, 2020

Jumatano, Aprili 29, 2020,
Juma la 3 la Pasaka

Mdo 8:1-8;
Zab 66:1-7 (K. 1);
Yn 6:35-40.

JE, MATESO YANA KUVUNJA MOYO?

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kufurahia baraka na neema zilizoletwa na sikukuu ya Pasaka na neno letu la Bwana katika somo letu la injili leo linatupatia matumaini makubwa sana. Anatuambia kwamba yeye ni mkate wa uzima na anayekuja kwake hakika hataona njaa kamwe. Anasema tena kwamba kila ajaye kwake na kumwamini hakika hatamtupa bali atamfufua siku ya mwisho. Ndugu zangu, Yesu ni mkate wa uzima kwanza katika Ekaristi takatifu ambapo ni yeye mwenyewe tunayempokea na kuja ndani yetu kutupatia uzima. Halafu, kwa neno lake tusikialo kila siku, neno hili huwa kwetu mkate wa uzima kwani ndilo linalotuongoza na kutuonesha sehemu ya kwenda kama mzaburi anavyotueleza kwamba “Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga katika njia yangu.” Yeyote yule anayekuja kwa Yesu kwa ajili ya kumpokea katika Ekaristi na halafu tena kwa ajili ya kuliruhusu neno lake liwe taa ya kumwongoza, hakika hatamtupa kamwe bali atamfufua siku ya mwisho. Hili tayari tumekwisha liona hasa kwa watakatifu kama akina Fransisko, Padre Pio na watakatifu wote: hawa walimpokea Yesu katika ekaristi na kulifanya neno lake liwe taa ya miguu yao na hakika walifaulu kwa kiasi kikubwa sana. Nasi ndugu zangu tusiache hata mara moja kuiheshimu Ekaristi takatifu na kulifanya neno la Bwana liwe taa ya kutuongoza.

Katika somo la kwanza tumesikia habari za jinsi wale wakristo wa kwanza wanavyoendelea kumtangaza Kristo mfufuka kwa watu. Jana tulimsikia jinsi shemasi stafano alivyoamua kumtangaza Kristo mfufuka kwa watu hadi kifo dini. Wayahudi walifikiri kwamba wakristo wangeogopa na kukimbilia sehemu nyingine. Lakini cha ajabu kumbe kile kitendo ndio kinachochea injili ihubiriwe Zaidi. Leo injili inapelekwa hadi Samaria na shemasi mwingine aitwaye Philipo. Na kilicho chochea hili ni kile kifo cha Stefano. Wayahudi walifikiri kwamba kwa kumpiga chura teke ndio wanamfanya aumie kumbe walikuwa wakimfanya aruke kwa kasi zaidi. Wayahudi walifikiri kwamba kwa kuumwagia maji moto wa petrol ndio ungezima kumbe hali ikageuka. Petrol ilipata nguvu na kutawanyika zaidi na ule moto kusambaa sehemu nyingi zaidi. Ndivyo ilivyo ndugu zangu, pale tutakapo onesha ukatili na uonevu kwa watu tukifikiria kwamba ndio watarudi nyuma wee-sio hivyo. Tambua kwamba unapomnyanyasa mtu, ndipo unamfanya aongeze bidii zaidi. Ni kama kumpiga chura teke-unamsaidia aruke vizuri zaidi. Hivyo, tuache ukatili na unyanyasaji hasa wa wadogo. Makaisari ya Kirumi kama akina Domitian na Nero walijaribu kuliangamiza kanisa na nguvu zao kwa kuamua kuwaua wale mitume wakuu kama akina Petro na Paulo-lakini kwa kufanya hivyo, Nero alijikuta anaufanya ukristo ukue tena kwa kasi Zaidi kwani vifo vya wale mitume wawili wakubwa viliwahimiza wale wakristo wengine wafanye bidii Zaidi kushuhudia ukristo wao. Hivyo, kama kuna yeyote anayejidai kulipinga kanisa labda kwa kuliibia fedha, kuliibia sadaka zake au kwa kulichafua, au kukataa kuhudhuria kanisani au jumuiya au hata kwa kulihujumu nakwambia jua kwamba ndio unalifanya lisonge mbele Zaidi. Kanisa lipo katika mkono wa kuume wa Mungu, ikiwa na Maana kwamba mkono wa kuume ni mkono wenye nguvu, hivyo lipo katika ulinzi mkali kabisa, usipoteze muda kusema unapigana na kanisa au kwakugoma kwako pengine labda kanisa litakufa. Lipo kwenye mkono wa kuume wa Mungu (Uf 1:6).

Maoni


Ingia utoe maoni