Alhamisi, Aprili 30, 2020
Alhamisi, Aprili 30 2020.
Juma la 3 la Mwaka
Mdo 8:26-40;
Zab 66:8-9,16-17,20 (K. 1);
Yn 6:44-51.
KUVUTWA KWA YESU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubhui ya leo. Leo bado tunazidi kujikumbushia juu ya habari zilizoletwa na Kristo mfufuka. Na katika somo letu la injili, Yesu anazidi kusema kwamba yeye ni chakula cha uzima, na yeyote atakayekuja kwake hakika hatamuacha bali atamfufua siku ya mwisho. Yesu anawaeleza kwamba yeye chakula atoacho ni tofauti na ile mana, ile mana walipoila kule jangwani waliila lakini pia wengi walikufa-ilishidwa kuwafikisha katika nchi ya ahadi. Hii ni kwa sababu ile mana haikuwa na nguvu, au neema iwezayo kumfanya mtu asonge mbele. Lakini chakula atoacho Yesu kinatoa neema, kinakupatia nguvu wewe mwenyewe usonge mbele. Chenyewe ni chanzo cha neema. Hii ndio Ekaristi Takatifu ndugu zangu, yenyewe inatoa neema, inakuunganisha na Mungu, na yeyote apokeaye Ekaristi, kwa moyo kabisa, na kwa imani, nakwambia mtu huyo si mchezo kamwangalie hata maisha yake, ni tofauti. Ekaristi ina nguvu ajabu lakini labda sisi hatujaitumia sawasawa kwa sababu tunafanyaga mambo kwa harakaharaka hasa kwa baadhi ya nyakati katika misa zetu. Lakini wale wakaa pweke au waherimita wa jangwani waliweza kuishi kwa kula tu ekaristi, waliweza kubakia na afya tele wakati wowote. Hivyo, sisi tuiheshimu Ekaristi vyema. Tuipokee, itufanye tubadilike na kuanza upya maishani hasa kwa neema itolewayo na hii Ekaristi.
Katika somo la kwanza, tumesikia habari za Philipo akimbatiza Towashi wa Ethiopia. Huyu alionesha nia na chembe ya Imani kwa kuanza kuyasoma maandiko matakatifu bila hata ya kuyaelewa. Lakini mara moja Mungu akabariki nia yake kwa kumletea mfafanuzi aliyemuelezea maana ya anachosoma na mwishowe Imani yake ikakua hata kubatizwa. Kama Yesu alivyosema kwenye injili hakuna aendaye kwake isipokuwa ni Mungu mwenyewe kamgusa na hili linatokea kwa Towashi huyu. Nasi tunaalikwa leo ndugu zangu, tuoneshe nia, tena kidogo tu, nakwambia Mungu atabariki mara moja, ukianza tu, Mungu naye anajalizia. Labda kama mimi ni mlevi na ninataka kuacha, hebu leo nisema basi sinywi -nakwambia utaona na Mungu mwenyewe atakuongezea nguvu ya wewe kuacha, au kama mimi siungamagi-nina miaka kumi na zaidi. Hebu leo niweke nia niseme nataka kuungama-utashangaa Mungu ataongezea ya kwake na utafanikiwa kuungama. Hivyo, ndugu zangu kwenye mambo mengi sisi tuweke nia tu nakwambia mambo utashangaa yakienda tu. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni