Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Aprili 28, 2020

Jumanne, Aprili 28, 2020,
Juma la 3 la Pasaka

Mdo 7:51-8:1;
Zab 31:3-4,6-8,17,21 (K. 6);
Yn 6:30-35.

YESU ANATOSHA KABISA
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana bado linazidi kutukumbusha juu ya maana ya pasaka, na neema tulizopokea kwa kipindi hiki cha Pasaka. Jana, baada ya Yesu kuwahimiza wale wafausi wake waliokuwa wanamfuata kwa lengo la kupata mikate ya kula kwamba watafute chakula kisichoharibika chenye kuwaletea uzima, sasa leo Yesu anapata fursa ya kuwaeleza viongozi wa Kiyahudi kwamba hata wao wanapaswa kungangania chakula hicho kisichoharibika na kumwomba Yesu awapatie chakula hicho. Yesu anawaambia kwamba chakula cha namna hiyo huwa kinaombwa kwani chatoka kwa Mungu. hata kile chakula walichokula kule jangwani ile mana, wasifikiri kwamba haikutoka kwa Mungu, Mungu ndiye chanzo cha ile mana. Lakini hii mana ilikuwa ni chakula kisicho cha kudumu-hivyo, katika injili hii, Yesu anawaambia kwamba waombe kile chakula kidumucho milele kiwezachokuwapatia uzima wa milele. Na hiki chakula ni yeye mwenyewe.

Ni kweli ndugu zangu Yesu mwenyewe ni chakula. Hili tunaliona katika fumbo la Ekaristi-hapa tunapata kumla Yesu kweli katika maumbo ya mkate na divai. Hii ekaristi ni chakula kiwafaacha wasafiri wote, sisi hapa duniani tunaoelekea katika nchi ya ahadi yaani mbinguni. Wakati waisraeli wakielekea katika nchi yao ya ahadi, walipewa mana toka mbinguni. Waliokataa kuila ile mana walikufa kwa njaa jangwani na kushindwa kufika katika nchi ya ahadi. Ndivyo na sisi ndugu zangu, sisi tulio safarini kuelekea katika nchi ya ahadi. Tunapewa Ekaristi tutakapokataa kuila, nakwambia tutashindwa kufika katika nchi ya ahadi yaani mbinguni. Nakwambia utashambuliwa na njaa, utashambuliwa na shetani, na utaishia kufa tu njiani. Na hii ni kweli. Wengi tunaokataa kula Ekaristi tunaishia kukata tamaaa au kufia njiani. Hivyo, ndugu zangu, tuiheshimu vyema Ekaristi. Tuwaheshimu na mapadre wetu pia.

Katika somo la kwanza tunakutana na kifo cha shemasi Stefano. Yeye kwa kitendo chake cha kukubali kufa shahidi kwa kumtangaza na kumtetea Kristo chaonesha kwamba yeye alimkubali Kristo. Alimuona kama chakula chake, alifurahishwa kulishwa neno lake na sakramenti zake. Nasi tunaoshiriki katika sakramenti hizi tunapaswa kuonesha ujasiri kama wa huyu Stefano. Si kwamba tunashiriki katika kumla Kristo na kwenye sakramenti zake halafu mwisho wa siku tunakuwa tena waoga, mtu akikuambia utoe hiki au ufanye utume Fulani unaogopa. Tujue kwamba Yesu katika Ufunuo anasema kwamba watu waoga hakika hawataingia katika ufalme wa Mungu (Uf 21:8). Hivyo tuwe na ujasiri

Maoni


Ingia utoe maoni