Jumamosi, Aprili 25, 2020
Aprili 25, 2020.
-------------------------------------------
JUMAMOSI, JUMA LA 2 LA PASAKA
SIKUKUU YA MT. MARKO, MWINJILI
Somo la 1: 1 Pet 5:5-14 Somo linaongelea kuhusu Marko, ambaye Patro alimchukua kama mtoto wake.
Wimbo wa Katikati : Zab 89: 2-3, 6-7, 16-17 Maisha yote midomo yangu itatangaza ukweli wako.
Injili: Mk 16: 15-20 Yesu anawambia wale kumi na mmoja waende ulimwenguni kote; wakahubiri kwa mataifa yote.
------------------------------------------------
KUJAZWA NEEMA NA KUTANGAZA NENO LA MUNGU KWA MAPENDO
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikukuu ya Mtakatifu Marko Mwinjili. Yeye hakuwa mtume wa Yesu lakini alikuwa mfuasi hodari wa mitume, hasa mtume Paulo na Petro. Kutoka kwao (hasa toka kwa mtakatifu Petro) aliweza kupata habari na mafundisho kumhusu Yesu. Hivyo, alijitolea kuandika habari za Yesu katika injili yake ya Marko. Yote haya aliyafanya kwa kujitolea tu; hakukuwa na mshahara wowote.
Katika somo la kwanza toka katika barua ya kwanza ya mtume Petro, Petro anamtaja Marko kama mwanawe mpendwa. Yeye aliambatana na mtakatifu Petro huko mjini Roma na aliandika injili yake akiwa na lengo la kuwataka wamfahamu Kristo na leo katika sehemu ya injili yake tunayoisikia tunasikia akiandika na kusisitizia juu ya umuhimu wa injili kwenye maisha ya watu na kwamba Bwana aliwatuma mitume ulimwenguni akiwaeleza kwamba kweli waihubiri na kuwabatiza watu na aaminiye na kubatizwa ataokoka. Ni Dhahiri kwamba Marko alipokutana na habari kama hizi zilimfanya akazane sana kuhakikisha kwamba injili inahubiriwa na ndio maana alikuwa tayari kuambatana na mitume na baadaye kuandika injili na kuhakikisha kwamba injili inamfikia kila mmoja. Yeye alikuwa mtu wa kwanza kuandika injili na yote haya aliyafanya kwa majitoleo tu na imani kubwa kama tunavyokutana na habari zake katika somo la kwanza kwamba alikuwa mfuasi mwaminifu wa mtume Petro.
Ndugu zangu, mwinjili huyu alitambua kwamba kanisa litaweza kusonga mbele kwa njia ya majitoleo tu, na ndivyo ilivyo. Hivyo alizidisha sana majitoleo. Injili aliyoiandika na safari zote alizoamua kuambatana na mitume hawa wakubwa, Petro na Paulo, yote haya aliyafanya kwa kujitolea, lengo lilikuwa ni injili isonge mbele. Nasi ndugu zangu tutambue jamani kwamba kanisa linajengwa kwa majitoleo-tukitegemea kwamba ati kila mtu alipwe bila majitoleo na Imani nakuambia hatutafika popote. Fikiria kama Mitume na Wenjili wangekuwa wanadaigi mishahara kwa kazi zao kweli wakristo wale wa mwanzo wangeweza kuwalipa? Au kama wamisionari labda wale waliokuja Afrika wangekuwa wanadaigi mishahara unafikiri jamii ya wakristo wangeweza kuwalipa? Au kama mapadre, maaskofu, masista, mabradha, makatekista, wanakwaya, wapiga vinanda, waalimu wa kwaya, viongozi wa jumuiya na hata baraza la walei kama hawa wote wangekuwa wanadaigi mishahara je, unafikiri wote wangekuwa kama serekalini unafikiri jamii ya Wakristo ingeweza kuwalipa? Jamani, kanisani ni majitoleo; pesa tusiziweke mbele, yaani ukishasikia kwamba kuna kazi ya kanisa yeyote inayohitajika kufanywa, cha kwanza weka majitoleo mbele. Ukiweka masuala ya faida na hasara nakwambia hatutafika popote.
Tafakari hii basi iwatie moyo wale ambao wanaendelea kujitolea kwa ajili ya kanisa, pia, iwatie moyo baadhi ya viongozi wa jumuiya na parokia, wale ambao wakati mwingine unawakuta wanapoteza hata masaa mengi wakimsubiri paroko awapatie mwongozo fulani au pengine wanapita kwa wana jumuiya wenzao kuhamasisha michango nakuonekana kama wasumbufu . Jamani tusikate tamaa. Iwatie moyo pia na mapadre wote na watawa wote na makatekista wote na viongozi wa baraza la walei na wa jumuiya; watambue kwamba kanisani ni majitoleo: si sehemu ya faida, wajue yote yanafanyika kwa ajili ya Mungu na si faida yao. Hivyo, pale ambapo labda pametokea watu wanaotaka kuwahamasisha wafanyakazi wa kanisani waende labda serekalini na kudai haki zao kisheria-sawa-lakini wenyewe kwa wenyewe lazima watambue kwamba majitoleo ni sehemu ya malengo yao katika Imani.
Maoni
Ingia utoe maoni