Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Aprili 24, 2020

Aprili 24, 2020.
-------------------------------------------
IJUMAA, JUMA LA 2 LA PASAKA

Mdo 5:34-42
Zab 27:1, 4, 13-14
Yn 6:1-15

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho Takatifu la Misa asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana bado linazidi kutukumbushia juu ya habari njema tuliyoletewa na Kristo mfufuka. Na siku ya leo katika injili tunamkuta Yesu akiwahubiria watu habari njema na kuwapa chakula. Yeye anatambua kwamba watu anaowafundisha ni binadamu, na tena wanasikiaga njaa-tena sana. Hili alilitambua na ndio maana baada ya kufundisha aliamua kuwapatia chakula. Kitendo hiki kinatufanya tuingie ndani ya mioyo yetu na kujipatia changamoto juu ya namna tunavyoongozaga njia zetu za maisha.

Utakuta mtu umeitisha labda semina yako unafundisha watu-tuseme wanakijiji-halafu cha ajabu ni kwamba yule mwongoza semina baada ya muda Fulani anakwenda mahali anapata kitu pale alipoandaliwa. Lakini wale wanaomsikiliza hawajaandaliwa chochote. Mwezeshaji anakwenda kula wao wanabakia wakipiga miayo. Namna hii sio nzuri. Au hata mwalimu unakuta shuleni anafundisha wanafunzi-yeye anajua baada ya muda fulani atakwenda kula, sasa je, wale wanafunzi anaowafundisha hatima yao hata haijulikani wale wasile hawajui. Namna hii sio nzuri. Ili tuweze kufanikiwa, lazima tuwe na ile hali ya kujali kila upande. Shule zinazofanya vizuri ni zile ambazo walimu wanajali-wanajua kwamba hata baada ya darasani wanafunzi wao watakula nini. Wale wasiojua wanachokula wanafunzi wao nakwambia watafeli tu. Au hata kama ni semina hata za kanisani-lazima kiongozi wa kiroho ajue kwamba waumini wake maswala ya chakula yanakuaje. Tusifundishe tu bila ya kujali hatma ya wale tuwafundishao. Wale viongozi wenye tabia ya kwenda kula na kuwaacha wasikilizaji wao wakiwa kwenye njaa-na baadaye wanarudi wakiwa wameshiba na kuanza kuwaambia wasikilizaji wao tuendelee, tuendelee, wee? waangalie tena hii namna yao. Jamani njaa inauma sana. Hivyo, mjali mwenzako aliye na njaa. Akikuambia kwamba ana njaa msaidie, usimwache aendelee kuumwa na maumivu makali ya njaa.

Halafu lazima tutambue kwamba mtu kuna wale wa ugonjwa wa kisukari-wao wakikaa bila kula kwa muda mrefu hupatwa na madhara Zaidi. Sasa, mtu akikuambia kwamba ana njaa-mjali. Yawezekana ni mwenye ugonjwa wa kisukari. Ile njaa yaweza hata kumfanya apoteze uhai, hivyo, usimnyime mtu msaada wa chakula bila kufikiria mara mbili ndugu yangu.

Katika somo la kwanza, tunakutana na mwalimu wa Kiyahudi akitoa ushauri kwa wazee wa Kiyahudi akiwaambia kwamba wafikirie mara mbili juu ya suala la kutaka kuwaangamiza mitume. Anawaeleza kwamba kama mpango wao umetoka kwa Mungu, hakika hawataweza kuushinda lakini kama umetoka kwa wanadamu, utakufa tu wenyewe. Huyu mzee alionesha hekima kubwa sana. Na kwa kweli dunia inahitaji akina Gamalieli wengi. Hii ni kwa sababu wengi wetu tunatumia nguvu sana, hatuna muda wa kufikiria, tunafikiri nguvu ndio zinazotupatia ushindi kila mahali. Sio kweli, kuna maswala yasiyohitaji nguvu bali hekima. Mfano, ukiwa mahakamani, unaweza ukawa wewe ndiwe umekosewa haki lakini kwa sababu ya kukosa hekima au kwa sababu ya kutaka kutumia tumia nguvu na kuforce mambo ukashangaa unashindwa. Hata katika kusoma-unaweza kutumia nguvu nyingi kusoma lakini ukafeli kwa sababu ya kukosa hekima. Hekima inahitajika katika kuishi na wenzako. Tuombe dunia iwe na akina Gamalieli wengi wawafunze watu hekima

Maoni


Ingia utoe maoni