Alhamisi, Aprili 23, 2020
Alhamisi, Aprili 23, 2020
Juma la 2 la Pasaka
Mdo 5:27-33
Zab 33: 2, 9, 17-20
Yn 3:31-36
KUJAA NEEMAA: NI KUISHI KATIKA KILE MUNGU ALICHOKUPA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana bado tunaendelea kusikia habari za Kristo mfufuka na tunaelezewa juu ya ukuu wa huyu Kristo ambaye katika pasaka hii amekuja kutukomboa. Yeye aliyekuja kutukomboa Yohane anatuambia leo kwamba ni mkuu kuliko wote, na yeye husema yale tu alioyaona na kuyasikia toka kwa Baba. Hivyo, kwa kweli anapewa upendeleo wa ajabu. Lakini cha ajabu ni kwamba licha ya kwamba ametutendea yote haya, wengi bado hawaisikii sauti yake. Hili tunaliona katika somo la kwanza ambapo wale viongozi wa dini ya Kiyahudi wanakataa na kukasirika wanaposikia kwamba mitume wanahubiri neno la Mungu na habari ya Yesu mfufuka na wanapanga hata kuwauwa. Lakini, Injili ya leo inatuambia kwamba anayemwamini Yesu anao uzima wa milele na asiyemtii Yesu atakumbwa na gadhabu ya milele. Sababu hizi zilieleweka vizuri masikioni na akilini mwa mitume tunaowasikia katika somo la kwanza na ndio maana leo wanasema kwamba hawawezi kuacha kumtii Mungu.
Hili ndilo aliko nasi ambalo Yesu anatuambia leo. Tutambue kwamba Yesu ndiye anayeokoa. Hivyo, tuoneshe hili kimatendo kwamba Yesu ndiye anayeokoa na hivyo lazima kumtii yeye kuliko mwanadamu. Kweli tunamtii Yesu kuliko mwanadamu? Mfano, mwajiri wako akakuambia kwamba usipokuja kazini jumapili basi nakufukuza kazi-je, utakuwa tayari kumjibu kama mitume wanavyomjibu kwamba lazima nimtii Mungu kuliko mwanadamu, yaani siwezi kuacha kwenda kanisani jumapili, je upo tayari? Au baadhi ya wenzako wasio waaminifu na wameiba mali kazini kwako-halafu wakakuambia kwamba ukitutaja basi tutakua-je, utakuwa tayari kusema kwamba mimi lazima kumtii Mungu kuliko mwanadamu? Au wewe ni mama wa ndoa na unashida kubwa sana za kifedha. Akaja Baba mmoja akaahidi kukusaidia lakini akakuambia kwamba masharti lazima ufanye uzinzi na yeye, je, utakuwa tayari kumwambia kwamba lazima nimtii Mungu kuliko wewe? Au kama wewe ni binti mwanafunzi na umepata ujauzito na kweli ujauzito huu utakufanya usiendelee na masomo na kuwafanya wazazi wako wakosane nawe, akaja rafiki yako akakushauri utoe mimba, je, utakuwa tayari kumwambia kwamba ni lazima nimtii Mungu kuliko mwanadamu? Au wewe una hali mbaya sana ya kifedha na pesa za wizi zinaletwa na wenzako wanaamua kukugawia na unajua ni kutoka kwa wezi, je, utakuwa tayari kuwaambia kwamba lazima kumpenda Mungu kuliko pesa zenu?Au kwamfano pia, umeajiriwa kwenye kampuni moja na bahati wewe ni Baba wa familia sasa mwenye watoto na gafla ukakuta katibu wako kazini kwako ni yule dada ambae alikuwa awe mchumba wako ikashindikana zamani, je sasa upo tayari kukaza macho kwa mkeo na kumtii Mungu?
Ukweli ni kwamba maisha yetu yanahofu na tunaogopa kumshuhudia Kristo kila wakati na kila siku tunakosa imani kwake. Sisi tutambue kwamba maisha yetu yafaa yawe mikononi mwa Bwana. Licha ya kwamba kuna shida zote hizo, basi tuyaweke mikononi mwake tu. Atatuongoza. Pale tunapo onesha udhaifu na kuanguka basi tusisahau kuomba msamaha.
Maoni
Ingia utoe maoni