Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Aprili 21, 2020

Jumanne, April 21, 2020.
------------------------------------------------
JUMANNE, JULA LA 2 LA PASAKA

Somo la 1: Mdo 4: 32-37 linaeleza maisha ya jumuiya ya kwanza na mambo yale mazuri yaliopatikana katika umoja huu.

Wimbo wa katikati: Zab 92: 1-2, 5 Bwana ni Mfalme, amejivika adhama.

Injili: Yn 3: 7-15 Sehemu hii ni mwendelezo wa mazungumzo kati ya Yesu na Nikodem na Yesu anatabiri kwamba atanyanyuliwa juu kama yule nyoka wa shaba.

------------------------------------------------

KUZALIWA UPYA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu; katika neno la Bwana, bado tunaendelea kuelezewa umuhimu wa neema tuliyoipokea kwa kipindi hiki cha Pasaka, bado tunafundishwa juu ya hiki tulichokipokea yaani maana halisi ya ufufuko na leo katika somo la Injili, tunakutana na Yesu akiendelea kumwelewesha Nikodemu umuhimu wa kifo chake kwa dunia na umuhimu wa kila mmoja kumwamini na kubatizwa katika jina la Yesu. Yesu anamwambia Nikodemo hadharani kwamba yeye ni zaidi ya yule nyoka wa shaba kule jangwani. Anapaswa kuangaliwa na kuabudiwa na kila mmoja, na yeyote takayekataa kumwangalia atakufa. Kweli haya mambo yalitendeka katika ile siku ya Ijumaa kuu ambapo Yesu aliinuliwa juu na sasa ni kwamba yeyote atakayekataa kumwangalia Yesu aliyeinuliwa msalabani kwa imani kweli hataweza kuupata wokovu.

Katika somo la kwanza, tunasikia namna jinsi jamii yote ya wakristo wa kwanza wale waliopata kumwangalia Yesu walivyogeuzwa maisha yao. Wao baada ya kumwangalia Kristo kama yule nyoka wa shaba, walipata uponyaji wa kila kitu, uadui uliisha, Kristo aliwafanya wasione faida ya kila mtu kungangania mali binafsi na hii ilisaidia kuondoa umaskini kati yao, Kristo aliwafanya wamwone kila mmoja kuwa ndugu, aliwafanya wasikie shida za wenzao, aliwafanya wasione mali kama ya lazima sana, wakawaona mitume kuwa ni kama baba zao na hivyo wakaweka kila kitu chini yao. Kwa kweli hii ilikuwa ni Imani kubwa ambayo kanisa hili na wakristo hawa walikuwa kati yao na kutokana na imani hiyo ama kweli walibarikiwa: mfano, miujiza mbalimbali ilitendwa kati yao, wenye magonjwa wakaponywa, watu wote wakawaheshimu sana, kanisa likaweza kukua. kwa mfano wao mwema, waliliwezesha kanisa kusonga mbele na kutuwekea msingi imara kwa ajili ya kanisa letu.

Isingekuwa mifano yao, hakika kanisa letu lingekosa dira.
Nasi ndugu zangu tuwe kama watu ambao ama kweli tumewahi kumwangalia Yesu kama yule nyoka wa shaba pale msalabani na kupata uponyaji. Tatizo ni kwamba kweli tunavyoishi ndani ya ukristo wetu, tuko kama watu ambao hatujapokea neeema yoyote toka kwa nyoka wetu wa shaba ambaye tunamuangaliaga kila siku yaani Yesu. Tunaishi bila kuaminiana mno, tunaogopana, tunaibiana na kudhulumiana. Mfano, mfanyabishara akimuona mkristo mwenzake hamuoni kama ndugu katika Imani bali anajaribu kutafuta namna atakavyomdanganya na kumuuzia kitu kwa bei kubwa. Hivyo, atatafuta maelezo ya uongo lengo ni kumdanganya auze bidhaa zake kwa faida. Na yule anayenunua vilevile-atatafuta namna atakavyomdanganya muuzaji labda kumwambia mama mgonjwa au nini na nini lengo likiwa ni anunue vitu kwa bei ya chini. Mwisho wa siku tunaishia kuogopana na kutooneana huruma. Au unaona mtu akiuziwa bidhaa feki ambazo kwa hakika hata wewe mwenyewe huwezi tumia lakini unakaa kimya. Au unanunua vitu vya wizi wakati unajua kabisa huyu kijana hawezi kupata vifaa hivi na hali yake hii. Mtu anakuuzia simu ya milioni moja kwa shilingi elfu hamsini lazima ufikirie usije ukawa unashirikiana na muovu kuendeleza uovu na kuharibu ile hali ya moyo mmoja na roho moja ndani ya dunia. Hivyo tuwe watu wa kuamininiana na kuona matatizo ya wenzetu. Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni