Jumamosi, Aprili 18, 2020
Jumamosi, Aprili 18, 2020,
Oktava ya Pasaka
Mdo 4:13-21
Zab 118:14-21
Mk 16:9-15
IMANI INATUONGOZA KWENYE UKWELI WA UFUFUKO!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kufurahia furaha iliyoletwa na Kristo mfufuka na leo tafakari ya neno la Bwana, injili yetu inatuambia kwamba tumtangaze Kristo mfufuka kwa wengine. Lakini kabla ya kumtangaza huyu Kristo, lazima uamini kwamba amefufuka na ndivyo uweze kuwaambia wengine kwamba Kristo amefufuka. Hili ni tatizo lililowakumba wale wanafunzi-baadhi yao kama tunavyoona katika injili hawakumuamini Kristo kwamba amefufuka na leo Yesu anawakemea kwamba waamini na ndipo waweze kupeleka habari hizi kwa wengine. Kristo mfufuka anayo nguvu ya ajabu-akishakutana na wewe lazima akubadilishe na kukurahisishia maisha yako, maisha yako kama alivyokutana na yule kiwete na kumrahisishia maisha yake. Zaidi ni kwamba hata mhubiri mwenyewe akishakutana na Kristo mfufuka na kuanza kumhubiri nakwambia anajikuta akibadilishwa kwa njia ya ajabu kiasi kwamba hakubali kabisa kuacha kumhubiri huyu Kristo. Hili ndilo lililowakuta mitume ambao tunawasikia leo katika somo la kwanza, wao hawakuwa tayari kabisa kumwacha Yesu-wako tayari kumhubiri hadi gerezani-yaani wameuonja wema wake, ukuu wake, ulinzi wake na hivyo hawataki kumwacha. Ndivyo ilivyo kwa yeyote aliyekutana na Kristo.
Fundisho hili linatoa onyo kweli hasa kama wakristo: jamani unashangaa kuona kwamba mtu alishawahi kukutana na Kristo, aliwahi hata kujiunga na ule utoto wa kipapa katika utoto wake, labda aliwahi kucheza kanisani na hata kusindikiza vipaji, wengine labda waliwahi kuwa hata watumishi kanisani-au kujiunga na shirika la Bikira Maria au kujiunga na Karesmatiki. Sasa unashangaa kuona kwamba ati mtu huyu sasa amebadili dini ili aoe au aolewe. Jamani, hamwonagi uchungu? Huyu mtu hakufurahishwa na Kristo aliyekutana naye kipindi hicho? Lazima tujue kwamba mtu wa namna hii kamruhusu muovu amchezee na ndio maana maishani wengi huishia katika kuhangaika tu.
Au unakuta mtu wakati akiwa kaajiriwa na pesa zipo, alikuwa muumini mzuri, kanisani kila siku, lakini kaona kwamba mambo yamemuendea vingine, basi, anaachana kabisa na kanisa, anaona Mungu hana kitu, je? Hukumbuki wema aliokutendea Mungu nyakati hizo jamani? Tuone uchungu kumwacha Kristo. Tukumbuke jinsi alivyowahi kututendea wema mkubwa na kuhakikisha kwamba kamwe hatumuachi-tuone haya kumwacha Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni