Jumatano, Aprili 15, 2020
Jumatano, Aprili 15, 2020.
Oktava ya Pasaka
Mdo 3:1-10
Zab 105:1-4,6-9
Lk 24:13-35
UFUFUKO: YESU YUPO HAI KATIKA EKARISTI TAKTIFU.
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tupo katika octava ya pasaka na tunaendelea kufurahia habari njema iliyoletwa na Kristo mfufuka. Na leo ujumbe wa neno la Mungu unaongozwa na wimbo wetu wa katikati kwamba nchi imejaa fadhili za Bwana, kitendo cha Yesu kufufuka na kuitangazia dunia matumaini ni dalili kwamba kwa kweli nchi imejaa fadhili za Bwana, yaani Bwana anaipenda nchi kwa kiasi kikubwa mno na ameshaijaza neema zake kwa kiasi kikubwa sana. Tangu auumbe ulimwengu, halafu mwanadamu akatenda dhambi na sasa akamtuma mkombozi aliyekuja kumkomboa mwanadamu kwa kumwaga damu yake na kufufuka. Hivyo, kweli nchi imejaa fadhili za Bwana na isingekuwa imejaliwa hizi fadhili, hakika ingaliangamia tayari. Hivyo, nchi imejaa fadhili za Bwana. Na leo sasa katika somo la kwanza, Petro anavyomponya kiwete kwa kutumia jina la Yesu, Yesu mfufuka ni dhihirisho la hizi fadhili za Bwana zilizojaa katika hii nchi. Hivyo, tusichoke kuomba kabisa, hii nchi imejaa fadhili za Bwana, kila tumwombapo Bwana msaada hakika atatupatia tu. Nchi imejaa fadhili za Bwana.
Basi, kama nchi imejaa fadhili za Bwana, basi nasi tushirikishane hizi fadhili. Shida ni kwamba watu hatushirikishani, unakuta mtu anamwaga chakula wengine wanakufa njaa, chakula kinapewa mbwa lakini wengine wanakufa njaa, pesa zinatumika kwenye kununulia pombe lakini familia inakufa njaa, watu wanapoteza pesa kwenye kumbi za starehe na disko za usiku lakini wazazi wao wanakufa njaa nyumbani. Huu ni utumiaji mbaya wa fadhili za Bwana. Tuzitumie fadhili za Bwana kwa kushirikishana na Injili yetu ya leo imetuambia kwamba Kristo anapatikana pale wawili au watatu wakusanyikapo na kuanza kushirikishana hizi fadhili. Hakika Kristo atakuja ndani yenu licha ya mapungufu mlio nayo, na kutuletea fadhili zake zaidi. Basi, kwa tafakari hiyo, tuongeze ushirikishanaji jamani wa fadhili za Bwana. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni