Jumanne, Aprili 14, 2020
Jumanne, Aprili 14, 2020,
Oktava ya Pasaka
Mdo 2:36-41
Zab 33:4-5,18-20,22
Yn 20:11-18.
UFUFUKO: WITO WA KUKUWA KATIKA MAHUSIANO NA YESU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu kwa siku ya leo. Bado tunaendelea kusheherekea na kufurahia neema ziletwazo na kipindi cha Pasaka. Ukweli ni kwamba kila tuikumbukapo Pasaka, tunapata kushiriki zile neema alizozitoa Kristo pale alipofufuka. Pale alimshinda shetani, akashinda kifo na hivyo basi na sisi kila tuadhimishapo Pasaka, tunaonyesha nguvu yetu juu ya shetani-kwamba hatumtaki na tunakataa uanachama naye. Halafu, pia tunapata nafasi ya kujikumbushia kwamba kifo hakina nguvu juu yetu na hivyo kama tutamtumainia Kristo, hakika hatutaweza kushindwa. Hii ndio furaha tuletewayo kila Pasaka. Leo katika somo la injili, tunakutana na Maria Magdalena akiwa kaburini katika uchungu mkubwa. Yeye kaja kuomboleza, alimpenda huyu Yesu, anakumbuka ule wema aliowahi kumtendea, jinsi Yesu alivyomuokoa na pepo waliokuwa wakimtesa. Sasa anakumbukia yote hayo, anakumbukia tena jinsi alivyoteswa na kuuawa-na sasa anaenda kaburini haikuti maiti yake-anafikiri imeibiwa tena-hivi vyote vinamuongezea uchungu na hivyo anaamua kulia tu. Sasa, akiwa katika uchungu huo, Yesu anamtokea na gafla huyu Mama uchungu wake wote unageuka kuwa furaha. Kweli kwa huyu Mama ilikuwa furaha kubwa, alizidi kuona uwezo wa Yesu, kweli sasa waliweza kusema Yesu no mkuu kweli. Kama ameweza kushinda tena kifo, basi kweli Yesu ndiye Masiha. Yeye anaambiwa akatangaze habari hizi kwa mitume.
Katika somo la kwanza, tunamkuta Petro akitangaza habari hizi kwa nguvu sana na anataka watu wamgeukie Yesu ili awapeleke katika yale matumaini ambayo yeye mwenyewe ameyaanzisha-na wale watu wanapohubiriwa wanachomwa mioyo na kujiunga na kuanzisha jumuiya ya kwanza ya Kikristo.
Ndugu zangu, hawa watu waliyapokea mafundisho ya Petro kwa moyo na ndio maana waliweza kuwa wafuasi wa kwanza na kuanzisha kanisa la mwanzo. Sasa tujiulize sisi, tumeshasikia mahubiri toka kwa watu mbalimbali, mapadre mbalimbali, hadi maaskofu, je, umekwisha anzisha jumuiya au makanisa mangapi? Labda nyie ni kigango, kila siku mnakubali msali katika kanisa lililojaa vumbi au lisilo na mabati, au lisilo na sakafu, au lisilo na umeme, au lenye paa la nyasi-sasa inamaanisha kwamba Wakristo wote wa hicho kigango au Parokia mmeshindwa kukazana na kufanya kitu? Mnakazana muweze kumtangaza Kristo au unangangana na nyumba zako tu na kuacha nyumba ya Mungu kuwa mahame? Wale wakristo wa mwanzo wangefanya ulelemama hakika wasingeweza kutujengea makanisa mazuri kama tuyaonayo sasa. Sasa siku hizi haya makanisa hayatoshi jamani, tujenge vigango haloo! Jamani! Lazima tujenge na tusilale. Na jumuiya za Kikristo jamani tukazane zikue. Tujitolee kwenye kazi za kanisa. Tufurahi kumtanga Kristo mfufuka kila mahali, hili liwe lengo letu jamani. Tusilalee, tuamke jamani, Kristo atangazwe kila mahali. Tusifikirie tu kujiserengetilize, na kujicastlelize na kujikitimotolize kila wakati. Tufikirie kwa moyo wote jinsi ya kumtangaza Kristo kama Wakristo wa mwanzo walivyokuwa na bidii kiasi kwamba hata kutoa maisha yao kwa ajili ya Kristo haikuwawia vigumu
Maoni
Ingia utoe maoni