Jumatano, Aprili 08, 2020
Jumatano, Aprili 8.2020
Juma Kuu
Isa 50: 4-9;
Zab 68: 8-10, 21-22, 31, 33-34;
Mt 26: 14-25.
KUBEBA MISALABA YETU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Mungu tunaendelea kumkuta Yesu akiwa katika uchungu mkubwa kwani mateso yake ambayo ni makali sana yamekaribia na yeye anazidi kuumia moyo sana. Na huzuni yake inazidi kuongezeka kwani yule ambaye aliwaonesha upendo, mmoja wao anapanga njama za kumsaliti na mwingine atamkana mbele ya watu licha ya kwamba yeye amekuwa akiwaonesha upendo siku zote. Zaidi sana katika injili ya leo, Yesu anakuwa katika karamu pamoja na wanafunzi wake. Karamu hii ilikuwa tena ni ishara ya upendo na wanafunzi wake wangalipaswa kujibu upendo huo kwa mapendo. Lakini wao hawakufanikiwa. Yesu anaamua kuwaeleza waziwazi kwamba mmoja wao atamsaliti, angetegemea kwamba suala hili lingewashtua wote na labda wangeitisha kikao na kuulizana na kusaidiana na kumkanya yule mwenye tabia mbaya za aina. Lakini cha ajabu hakuna kikao walichoitiana; walichukulia suala hili kuwa ni mzaha. Nafikiri walikuwa hata hawamwonyagi yule Yuda ambaye walikuwa wanajua kwamba alikuwa ni mwizi. Sisi ndugu zangu tutambue kwamba wajibu wetu pia ni kuonyana sisi kwa sisi. Vitu vingi vinaharibika kwa kuwa tunaogopana, hatuambiani ukweli, hatufuatilianagi mambo yetu, hadi pale mambo yanapoharibika ndio tunashtuka. Tusiwe wanafiki ndugu zangu. Tabia kama hizi tuziache, zinawafanya wenzetu wapotee na wengine kuumia.
Katika somo la kwanza, tutakutana na habari ya mtumishi mwaminifu wa Mungu aliyempole na kukabali hata kuutoa mgongo wake upigwe. Huyu alikuwa ni Yesu ambaye kwa kuutoa mgongo wake upigwe, ndio alivyoweza kuwaokoa wengi. Nasi tutambue kwamba kama hatutakubali wakati mwingine kuutoa mgongo wetu upigwe, yaani wakati mwingine kukubali kuonekana kama mjinga, yaani wakati mwingine nikubali kuumia na kupoteza-nasi kwamba ati kila siku mimi nitaonekana kuwa mjanja mwenye kuweza kupata faida, kama hatutaweza na sisi kuwa namna hii ya Yesu, hakika nakuambia hatutaweza kumfikia na kumhudumia mwenzetu. Kuweza kumhudumia mwenzetu yabidi tukubali kupoteza na wakati mwingine tuonekane kuwa wajinga. Kujishusha na kuwahudumia wadogo. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni