Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Aprili 06, 2020

Jumatatu, April.7.2020
Juma Kuu

Isa 42: 1-7;
Zab 27: 1-3, 13-14;
Yn 12: 1-11.

HARUFU NZURI YA UPENDO!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tayari tumekwisha ingia wiki kuu na takatifu, tafakari ya neno la Bwana leo injili inazidi kuonyesha uadui uliopo kati ya Yesu na viongozi wa dini ya Kiyahudi; katika injili tulizosikia, wao walishashindwa kumwua kwa mawe na sasa watajaribu kushiriana na baadhi ya rafiki zake wa karibu ili wampate na injili ya leo inaonyesha vilema, udhaifu wa yule atakayemsaliti-kwamba alikuwa mpenda pesa na kilema hicho kitatumika ili kumwangamiza Yesu. Lakini kama linavyotueleza somo la kwanza, Yesu alikuwa yule mtumishi mwema, ambaye hatafifia au kufa moyo. Huyu mtumishi mwema anaonesha kwamba hakuwa na kilema au udhaifu fulani: angekuwa na udhaifu Fulani asingaliweza kutuletea ukombozi-tukumbuke kwamba shetani alikuwa anakuja mara kwa mara hasa zile nyakati za shida kwa Yesu kutafuta udhaifu ili amteke na kumwangusha Yesu. Lakini anashindwa. Sasa ataamua kutumia moja ya udhaifu wa wanafunzi wake.

Ndugu zangu, tuitumie wiki hii vizuri; hii ni wiki ya kuangalia jinsi vilema vyetu vilivyotumika kutufanya tutende dhambi, kusaliti nadhiri zetu za kitawa, maagano yetu ya ubatizo, na ndoa. Tamaa zetu zinatufikisha pabaya. Angalia namna shetani alivyoweza kutumia tamaa yako ya pesa, tamaa yako ya vinywaji, tamaa yako ya wanaume au wanawake, hasira zetu, ulafi ili kukufanya utende dhambi. Tumwombe Mungu msamaha kipindi hiki

Maoni


Ingia utoe maoni