Jumanne, Aprili 07, 2020
Jumanne, April.7.2020
Juma Kuu
Isa 49: 1-6;
Zab 71: 1-6, 15, 17;
Yn 13: 21-33, 36-38.
KUWA HURU KUMCHAGUA YESU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo katika tafakari ya neno la Mungu tunamkuta Yesu akiwa katika uchungu mkubwa kwani muda wa mateso yake ambayo ni makali sana unakaribia na mbaya zaidi ni kwamba yule atakayemsaliti ndio leo sasa anatoka hadharani mbele ya Yesu na kwenda kumsaliti kwa wakuu wa makuhani. Lakini Yesu bado kabakia akiwa hana uadui na mtu na hata yule ambaye anamsaliti anampatia tonge-lile tonge lilikuwa alama ya upendo wa Yesu kwake akimwonesha kwamba bado anampenda, likionesha jinsi Yesu asivyo na uadui na Yuda. Tulitegemea Yuda ashtuke na afikirie mara mbili kitendo chake lakini cha ajabu ni kwamba Yuda anapokea tonge, anakula halafu mara moja anakwenda kumsaliti. Tamaa za Yuda zilikuwa zimemtawala kiasi cha kushindwa kuona alama ya upendo aliouonesha Yesu kwake. Hadi hapa Yesu haangaiki bali anazidi kumlilia Mungu kama zaburi ya leo inavyotuongoza.
Hapa tuna mambo makuu ya kujifunza: kumlipa baya yule aliyekutendea mema ni miongoni mwa mambo mabaya sana. Kuna wakati unakuta labda mama yako au jirani zako walikusaidia halafu gafla wewe ukakua na kuanza kumpiga mama yako au kumnyanyasa. Wema aliokuonesha muda wote unausahau. Au unakuta mtu alikupokea kazini wakakusaidia wakati ukitafuta ajira, wakakuajiri halafu wewe inafika wakati umezoea kazi unaanza kuwadharau na kuwaibia au kukataa kufanya kazi na kuonesha uvivu. Au wakati wa kutafuta mke au mume ulikuwa mnyenyekevu lakini sasa umeshaolewa au kuoa na kuzoea ndio unaanza majivuno. Hii ni kulipa wema kwa baya. Unakumbukia jinsi alivyokusaidia? Halafu ndio sababu za kujivuna? Au unakataa hata kumtambulisha Baba au Mama yako kwa marafiki zako kwasababu hawana uwezo, wewe ni kuwatambulisha Baba wadogo, mashangazi kwasababu wanajua kuvaa suti na wana kipato kizuri.Angalia vyema.
Katika somo la kwanza tunasikia habari za mtumishi mwema. Yeye ndiye ambaye ataweza kuwafanyia watu hukumu na kuziinua kabila za Yakobo kwani yuko tayari kuyatoa maisha yake kwa ajili ya wengine. Yesu anatimiza unabii huu wa mtumishi mwema kwani yuko tayari kuyatoa maisha yake kwa wengine. Hakuwa mtu wa kupiga sana kelele bali utambi utoao moshi hakuuzima. Sisi nasi tujifunze kutokuuzima utambi utoao moshi. Wapo wengi wenye madhambi yao tusiwatenge na kuwakataa, tuwasaidie waweze kuacha na kwenda mbele. Wengi kati yetu ni kuzima utambi utoao moshi, mtu mwenye shida havumiliwi, hakuna mwenye utayari wa kukubali kuyabeba mateso ya mwingine-ndio maana kila siku wezi wanauawa, wagonjwa wanakufa mahospitalini na watu wanakufa njaa. Ni kwa sababu tunazima tambi zitoazo moshi (wale dhaifu kabisa ambao ni kama utambi unaotoa moshi ukijiandaa kuzima kabisa-tuuwashe kwa kuwasaidia na sio kuukanyaga na kuuzima kabisa-kuwaonea) . Hatujui kwamba hata sisi hapo mwanzo tuliwahi kutoa moshi- Sisi tuwe tayari kuyabeba kama Yesu alivyobeba ya kwetu. Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni