Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Aprili 03, 2020

Ijumaa, Aprili 3, 2020
Juma la 5 la Kwaresima

Yer 20: 10-13;
Zab 17: 2-7;
Yn 10: 31-42.

IMANI ILIYO JARIBIWA

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari ya neno la Bwana katika injili tunaendelea kukutana na mwendelezo wa hali ya kutokuelewana kati ya Yesu na Wayahudi na mambo yameshaonekana hadharani kwamba lengo la viongozi hawa ni kumteketeza Yesu kwani leo na jana wameinua mawe kabisa kutaka kumpiga. Kanisa leo limepanga somo la kwanza kwa namna ambayo litatufanya tuingie katika mateso ya Yesu. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha nabii Yeremia tunakutana Yeremia akimlilia Mungu amuokoe kwani amekosa mtu wa kumwokoa, kumtetea ndani ya ile jamii ya Kiyahudi. Yeye kila mtu amepanga kumteketeza, hata wale aliowategemea wamlinde, watu wa nyumbani mwake, wamemgeuka kabisa; hivyo hana msaada na anamuomba Mungu amwokoe kwani yeye ndiye msaada wake tu. Hali hii iliyompata Yeremia katika injili sasa tunakuta ikimkuta Yesu katika ukamilifu mkubwa kabisa. Yeye alikuwa ni wa familia maskini tu, anahubiri neno la Mungu, sasa wengi, hasa wale wenye nguvu wanamkataa na wameshampangia mipango ya kumteketeza. Hivyo, Yesu hana lolote licha ya kumlilia Baba kwani mipango imekwishapangwa ya kumteketeza na leo anataka kupigwa mawe hadharani kwa kuongea ukweli, kwa kufundisha mafundisho safi kabisa.

Ndivyo ilivyo ndugu zangu. Katika masomo haya, tumshukuru Mungu aliyekubali kujitoa kwa ajili yetu sadaka. Pia tujiangalie na hali yetu. Nasi pia tunao maadui kila mahali; labda wengine wananguvu zaidi yetu, wanapambana na wewe kama Yeremia au Yesu na unajua kabisa kwamba hawa watu nikipambana nao sintashinda, au hili tatizo nikipambana nalo sintashinda. Mkimbilie Mungu ndugu yangu. Hawatakushinda. Lakini ukimkosa Mungu, watakusumbua, watafanya propaganda ajabu hata za uongo kukuteketeza. Wengine labda tulikwisha inuliwa mawe na maadui wetu katika wakati Fulani, lakini tukashida, tumshukuru Mungu kwa hili. Pia somo hili tumsikiapo Yeremia akimlilia Mungu na Yesu akilalamika mbele ya Wayahudi na baadaye kumwachia Mungu, ndivyo wale tunavyowadhulumu, kama mayatima au wajane wakimlilia Mungu wanavyosikilizwa na sisi kama tutakuwa hatujaungama unashangaa tunapewa kadhabu ya maana. Hivyo, usimwonee yatima, akimlilia Mungu ndivyo pigo litakavyokugeukiaga. Au usimdhulumu yeyote yule.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni