Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Aprili 05, 2020

Jumapili, Aprili 5, April 2020.
Juma Kuu

JUMAPILI YA MATAWI

Mt 21:1-11 (Kutangaza ujio wa Bwana, Baraka ya matawi)

Isa 50: 4-7;
Zab 22: 8-9, 17-20, 23-24;
Fil 2: 6-11;
Mt 26:14 - 27:66.


MUNGU WANGU, MUNGU WANGU, MBONA UMENIACHA!

Leo ni jumapili ya matawi au jumapili ya mateso. Kipindi cha kwaresima tulicho kianza Jumatano ya Majivu, kinapata nguvu kwa liturjia ya juma hili na kilele chake kwa jumapili ya Pasaka. Kuanzia leo, liturjia zitakuwa zimejazwa na ishara na alama mbali mbali: matawi, kuoshwa miguu, nk. Tusikubali ibada hizi zipite machoni mwetu kama tu ishara ya nje pekee bali tuzichukue kama nafasi ya kuchunguza Imani yangu, ukweli na uhusiano wangu na Mungu.

Jumapili ya matawi inaonesha shangwe juu ya Yesu akiwa anaingia Yerusalem. Liturjia ya leo tunakumbwa na hisia mbili tofauti. Tunaanza lirtujia yetu kwa utukufu na shangwe kuenzi jinsi Yesu alivyo ingia Yerusalemu kwa shangwe kwa kuimba ‘hosanna, hosanna juu mbinguni’. Watu walifurahi kumuona Yesu alivyo ingia Yerusalemu kwa shangwe, lakini hali hii inapotea taratibu baada ya kuanza kuingia kwa undani katika masomo yetu hali inabadilika na kuwa ya kustua na huzuni. Injili inaishia na kutundikwa kwa Yesu msalabani na Yesu analia kwa sauti kuu nakusema “Mungu wangu mungu wangu, mbona umeniacha” na baada ya hayo Yesu anatoa pumzi yake ya mwisho na kukata roho. Kwa muda huu watu wote hupiga magoni kwa ukimya kutafakari kifo cha Yesu. Ni kwa jinsi ghani mambo yanaweza kubadilika kwa muda mfupi? Ni nini kilitokea kwa watu ambao walikuwa wakishangilia na kumsifu alivyokuwa anaingia Yerusalemu? Waliruhusuje, mtu huyu aingie katika mateso ya msalaba na kufa?

Jibu la ndani na la kweli kabisa kwa swali hili ni kwamba Baba aliruhusu haya yatendeke. Baba aliruhusu wamkane na kuruhusu asulubiwe. Yesu alikuwa na uwezo wakuonesha nguvu zake za Kimungu na kukataa kukumbatia mateso ya msalaba. Lakini hakufanya hivyo. Bali aliingia katika mateso na kukataliwa. Na wala hakufanya kwa kujutia au akilalamika. Aliyafanya kwa mapezi yake na kuyachagua kwa mapenzi yake.

Leo somo la kwanza linaeleza kwa undani kwamba, Yesu ni “Mtumishi wa Bwana anayeteseka”. Alijifunza kutii kwa njia ya mateso na kwa ajili ya utii wake, Mungu alimkweza juu kabisa. Alikuwa mtii hata kufa! Kila mkristo anatakiwa kupata nguvu kutoka katika njia ya Kristo. “Niliwapa mgongo wangu walio nipiga” somo la kwanza linasema. Hali ileile ambayo Yesu, mtumishi wa Mungu aliyeteseka ikatusaidia sisi wote. Hakurudisha kisasi, hakulalamika, wala kulaumu au kujionea huruma. Yesu aliyaangalia mateso na uchungu kama njia ya kuonesha upendo wake kwa Baba na upendo wake kwetu.

Mateso ya Yesu, yanatuonesha hisia, tabia na mtazamo wa watu. Kwa wakati mmoja walikuwa wamebeba matawi mikononi, wakitandaza nguo zao, wakiimba hosanna mfalme na siku chache baadae wanakuja kupiga tena kelele, ‘asulubiwe’ kwa Pilato. Kwanini, Mungu Baba aliruhusu haya? Kwa nini Yesu alichagua mateso na kifo? Kwasababu ndani ya hekima kamilifu ya Baba, mateso na kifo yalikuwa kwa lengo kubwa. Mungu aliamua kuaibisha hekima ya ulimwengu huu kwa kutumia mateso na kifo kama njia kamili ya kupata utakatifu. Kwa tendo hili, alibadilisha uovu mkubwa kuwa wema mkubwa. Msalaba unaninginia katikati mbele ya makanisa yetu na nyumbani kwetu, kuonesha kwamba hakuna hata uovu uwe mkubwa kiasi ghani unaoweza kushinda nguvu, hekima na upendo wa Mungu. Mungu ana nguvu kuliko kifo chenyewe na Mungu ana ushindi wa mwisho hata baada ya yote kuonekana yamepotea. Juma hili litupe matumaini ya Kimungu mara nyingi tunaweza kusukumwa kukata tamaa na mbaya zaidi tunaweza kushawishika kukata tamaa kabisa. Hakuna ugumu, hakuna msalaba unaweza kutushinda kama tutabaki waaminifu kwa Yesu Kristo tukimruhusu yeye abadilishe maisha yetu kwa utukufu aliokumbatia msalabani.

Ilikuwa ni watu kama Maria, Mama yake, mtume mwaminifu kama Yohane na wengine wachache walioweza kusimama pembeni nje ya kundi na kusimama karibu na Yesu. Katika mwanga wa simulizi la mateso ya Yesu na matukio mengine katika maisha ya Yesu ambayo yatasikika katika juma hili, tunapaswa kujitambua wenyewe. Je, mimi ni Mkristo wa makundi tu au Mkristo tu tukiwa wengi? Je mi ni Mkristo tu pale ninapo pata pato Fulani au sifa Fulani? Je, mimi ni muoga kusimamia ukweli?

Sala:
Bwana, ninapojaribiwa mpaka kukaribia kukata tamaa, naomba unipe matumaini. Nisaidie niweze kuona uwepo wako katika kila kitu, hata katika vitu ambavyo vinanisumbua mimi. Ninaomba juma hili kuu, libadilishe nyakati zangu za giza na mapungufu ninapo jikabidhi kwako, Mungu wangu. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni