Jumanne, Machi 31, 2020
Jumanne, Machi 31, 2020,
Juma la 5 la Kwaresima
Hes 21: 4-9;
Zab 101: 2-3, 16-21;
Yn 8: 21-30.
UHUSIANO WETU NA MUNGU
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Mungu baada ya kupumzika kwa ile siku ya jana ambapo tulitafakari juu ya mtakatifu Yosefu na kuona jinsi alivyotufundisha hasa sisi wanaume hasa wenye ndoa, sasa tunarudi katika mood ya kwaresima ambapo tunaendelea kusikia juu ya hali ya kutokuelewana kati ya Yesu na baadhi ya viongozi wa Kiyahudi na mipango ya kumteketeza Yesu inazidi kusukwa na leo baada ya kuwaona kwamba wao wenyewe wanakataa kumsikia na kuja kwake waponywe, anawaambia kwamba watakufa katika dhambi zao wenyewe-na katika kuelezea maada hii kwamba asiyempokea Yesu hufa katika dhambi zake mwenyewe, kanisa leo limechagua somo la kwanza linalotoka katika kitabu cha Hesabu lielezealo jinsi nyoka yule wa shaba alivyoweza kuwaokoa baadhi ya wana wa Israeli waliokuwa wamemkosea Mungu Imani. Musa aliambiwa atengeneze nyoka wa shaba na yeyote aliyekataa kumwangalia aliangamia. Leo kanisa linatumia somo hili kusisitiza kwamba Yesu anakaribiwa kunyanyuliwa juu na hivyo, yeye ni zaidi ya yule nyoka wa shaba na atakayekataa kumwangalia, hakika atakufa kutokana na dhambi zake, kwani nyoka wa sumu watamuuma kama walivyowauma wana wa israeli kwa sababu ya dhambi zao na walipona tu kwa kuitazama ile nyoka ya shaba. Leo katika injili tunasikia kwamba baadhi ya viongozi wa Kiyahudi wanakataa kumsikiliza Yesu na wanaambiwa kwamba watakufa katika dhambi zao. Hii yamaanisha kwamba kila mtu ni mdhambi na dhambi ndiye nyoka wa sumu na ni Yesu tu ndiye atakayeweza kumwokoa. Atakayekataa kumwangalia basi atakufa katika dhambi yake.
Sisi tunaposika habari hizi, tujue tufurahi kwani zamwonyesha jinsi Kristo wetu alivyo na nguvu na pia alivyo na uweza mkubwa kati yetu na jinsi awezavyo kutuokoa. Sisi nasi tuwe nyoka wa shaba kwa wengine, watu tutakaowafanya wengine wasife katika dhambi. Usimfundishe mwenzako dhambi au ukaidi wowote. Halafu, tuache majivuno, tusikubali kufa kwa ajili ya dhambi zetu wenyewe kama tuambiwavyo leo ndugu zangu. Mtu akikuambia ungama, kubali, usionyeshe majivuno na kumwambia usihangaikie maisha yangu au mambo yangu hayakuhusu. Tukijibu hivyo tunakuwa kama hawa Wayahudi ambao leo wanaambiwa kwamba watakufa katika dhambi zao wenyewe.
Maoni
Ingia utoe maoni