Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Aprili 02, 2020

Alhamisi, Aprili 2, 2020.
Juma la 5 la Kwaresima

Mwa17: 3-9;
Zab 104: 4-9;
Yn 8: 51-59.

AGANO LA UPENDO!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari ya neno la Bwana tunaendelea kusikia juu ya mwendelezo wa hali ya kutokuelewana kati ya Yesu na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiyahudi na leo mambo yamefikia mazito kabisa; Yesu kawaambia ukweli ambao hawakutaka kuusikia kabisa na kwa ukweli wanamweleza dhahiri kwamba tunataka kukumaliza sasa hivi, hakuna haja ya kusubiri tena-wananyanyua mawe na kutaka kumwangamiza. Hili ni dhihirisho kwamba hakika mioyo yao imeshachoka kumsikiliza Yesu na hivyo watamwangamiza tu. Mpangilio wa masomo yetu katika siku ya leo, somo la kwanza linazungumzia habari za Abrahamu. Somo linaonesha kwamba alibarikiwa na Mungu na kwa njia yake dunia nzima iliahidiwa baraka na yeyote atakayemfuata Abrahamu aliahidiwa kubarikiwa. Mungu alimpenda Abrahamu na alifanya naye agano kudhihirisha hili. Sasa katika somo la injili, Yesu anasema kwamba Yeye tena ni mkuu zaidi ya Abrahamu, hivyo, yeyote ambaye atajitahidi na kuwa moja kati ya mzao wa Kristo, ataweka agano maalumu na Mungu na hivyo atapokea Baraka, tena nyingi zaidi ya zile ambazo waliahidiwa wazao wa Abrahamu hapo mwanzo. Yesu anapokufa msalabani,anatukomboa katika utumwa wa shetani na kutufanya kuwa wana wa Mungu na wana wake. Hii inatufungulia mlango wa Baraka nyingi ajabu, zaidi ya zile hata za wana wa Abrahamu wa mwanzo. Hivyo ndugu zangu tuongeze Imani yetu kwa Yesu.

Tumshukuru kwa sababu alikubali kufa kwa ajili yetu na tumwombe azidi kutubariki Zaidi na zaidi. Kipindi hiki ni kipindi cha kukumbuka kwamba Yesu kwa kufa kwake aliachilia milango mingi ya Baraka. Sasa mimi najitahidi vipi kushiriki katika Baraka hizi? Kweli kuna neema yoyote niipatayo kwa kuadhimisha kifo cha Kristo? Kama hupatagi jua kwamba una shida. Rekebisha mambo ndugu yangu. Tumia vipindi vya sala vizuri, ungama vizuri, saidia maskini, usiwe na chuki na mtu. Hiki ni kikwazo. Kumchukia mtu ni kujifungia Baraka. Usionee mtu, tusitukane au kudhulumu, usimsengenye mtu, usiwe mmbea. Kingine ni wale tujionao kana kwamba ati sisi ni wahukumu pamoja na Mungu, wale tunaoshinda tukisali, tukifikiri ati kwamba tunamuungano na Mungu. Tuwe makini na hilo. Unyenyekevu ni wa muhimu. Yesu anasema hajitukuzi mwenyewe-tuache Mungu atutukuze. Tuombe Mungu atuongoze. Tusipofanya hivyo, usishangae kumkuta mtoto mdogo akikuzidi katika mambo mengi, akili na hata pia kiroho. Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni