Jumatano, Aprili 01, 2020
Jumatano, April 1, 2020
Juma la 5 la Kwaresima
Dan 3: 14-20, 24-25, 28;
Dan 3: 52-56;
Yn 8: 31-42.
UHURU KWA NDANI YA KRISTO!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari ya neno la Mungu inaendelea kutuweka zaidi kwa ajili ya kuyakaribia mateso ya Kristo, inatuonesha kwamba Kristo tayari amekwishajitoa mhanga kwa ajili yetu. Katika injili, tutasikia hali ya kutokuelewana kati ya Yesu na baadhi ya viongozi wa Kiyahudi na mipango ya kumteketeza inazidi kusukwa kila siku. Tafakari ya somo letu la kwanza inamfananisha na wale vijana watatu, Shadrak, Meshak na Abednego waliongangania kuiitii amri ya Mungu kiasi kwamba walikubali kufa kuliko kuitii amri ya Mfalme. Wao waliona kumtii Mungu kuna faida Zaidi. Imani yao iliwaweka huru na Imani hii iliwatetea kiasi cha kuwakinga na hatari ya moto wa mfalme. Moto ule haukuwaangamiza. Hali hii ndiyo ambayo kwa sasa ndugu zangu tunaikaribia kipindi cha mateso ndio itakayompata Yesu. Naye hatachoka kuwaambia wale wakuu wa Kiyahudi juu ya mafundisho ya kweli. Na yeye hatachoka kuyatetea mafundisho ya kweli. Nao watakasirika na kuamua kumuua lakini Imani ya Yesu na muunganiko wake na Baba itamuokoa kama ilivyowaokoa wale vijana watatu.
Ndicho anachotufundisha na sisi ndugu zangu. Anatuambia kwamba ukweli utatuweka huru-kamwe tusiogope vitisho, dhuluma, au vitisho vyovyote vile. Sisi tumtii Mungu. Yeye ndiye atakayetuokoa. Duniani tutakutana na maadui, tena wengi, lakini tukiyaweka matumaini yetu kwa Mungu, hakika tutashinda.
Lakini kama hututakuwa na imani, nakwambia hawa maadui watakutesa wewe-labda wataleta vyakula vyao na kuja kulia mbele ya macho yako ili wewe uaibike na kusalimu amri na kuwaomba. Watafanya masherehe yao, wataenda hata kukopa pesa na kwenda kufanya masherehe yao mbele ya macho yako ili ati wakuangushe wewe tu. Watavaa manguo yao, labda majinsi yao na maviatu yao ya bei na kukuringishia ili wewe usalimu amri. Watakusengenya, utachafuliwa popote, watasambaza chuki mbaya ili usipokelewe popote. Watakuringia, watakunyanyasa, watakufanya ujione mdogo na mwishowe unaweza hata kuwaomba msamaha. Lakini ukiyaweka matumaini yako kwa Mungu, hakika utashinda tu kama Kristo aliyetukanwa lakini hakujibu kwa tukano na baadae akashinda na kuleta ukombozi.
Maoni
Ingia utoe maoni