Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Machi 28, 2020

Jumamosi, Machi 28 , 2020,
Juma la 4 la Kwaresima

Yer 11: 18-20;
Zab 7: 2-3, 9-12;
Yn 7: 40-53.

KUMSIKILIZA YESU

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa asubuhi ya leo. Leo katika tafakari ya neno la Bwana tunaendelea kukutana na mipango ya kumwua Yesu bado ikiendelea na hali bado inazidi kuwa tete na Yesu naye haogopi kwani amekwisha kaza moyo wake kama gumegume kwamba atatetea mafundisho ya kweli na mwishowe atakufa kwa kutungiwa mashauri ya uongo kwani watashindwa kumkamata kwa kosa lolote.

Leo basi kama sehemu ya kuendelea kutafakari juu ya namna jinsi Kristo alivyojiandaa na kuwa tayari kutoa uhai wake, somo letu la kwanza linatupa habari za Yeremia. Huyu alikuwa nabii katika Israeli ambaye alikuwa anaililia Israeli itubu ili iokolewe na Bwana. Alijitoa kabisa kabisa kwa nguvu zake zote na kuwaambia watu kwamba watubu na waachane kuitegemea Misri wakidhani kwamba itaweza kuwaokoa mikononi mwa mataifa makali kama Babuloni. Hivyo alitumia nguvu zake zote akifundisha ukweli. Sasa yeye anafikiri kwamba anatenda jambo zuri kwa taifa kumbe bwana kuna watu wamejificha, wana hila mbaya na hawa watu ni ndugu zake kabisa kabisa wanataka kumwangamiza kwa siri-na hawa ni watu wa nyumbani mwake, watu aliowategemea wamlinde lakini wamemgeuka. Hivyo, Yeremia anamlilia Mungu na kumwambia kwamba ee Mungu usiniache, niangalie, mimi niko safi sina hatia, sijui kitu kabisa na kumbe kuna walionifichia mpango wa kunimaliza. Angalia ee Mungu, mimi sina nguvu yoyote hivyo niokoe.

Yaliyomtokea Yeremia ndugu zangu yanamtokea Yesu katika Injili ya leo. Mpango huu mbaya na wa siri unafanana na ule tunaousikia katika Injili ya leo. Leo tunasikia kwamba Yesu leo anahubiri zake, anafundisha watu mafundisho ya kweli, ana lengo zuri la watu waokoke na wamjue Mungu na kumwabudu kiaminifu na kumbe kati yake kuna watu wenye mpango mbaya ambao tena wametumwa ili wamkamate na kumwangamiza. Hii ilikuwa jambo la huzuni kubwa sana kwa Yesu, anatenda mema na yeye anapokea mabaya.

Somo hili ndugu zangu linatoa onyo kali hasa kwetu sisi ambao wakati mwingine tunakuwaga na mpango wa siri kwa wale ambao wanatutegemea. Unakuta mtoto kichanga kiko tumboni mwako wewe mama, kametulia zake, kanafurahi, kanazungukazunguka huko kakijua kwamba kiko salama ndani ya tumbo la mama, sasa wewe unakapangia mpango wa siri wa kukiangamiza-jamani kale katoto kanajisikiaje? Kamekutenda nini? Jiulize je, akimlilia Mungu kama Yeremia anavyomlilia Mungu leo dhidi ya hawa wapangao mipango michafu utasimama? Au wewe mwenyewe mtu kakuamini-labda mke wako au rafiki halafu akakuambia siri yake, siri kubwa labda ya ugonjwa wake au kitu fulani. Anategemea uiweke, umtunzie ili aishi salama kwa Amani mbele ya watu-sasa wewe unakwenda kuisema na kumfanya yule mtu ashindwe kutembea mbele ya jamii-jamani huyu mtu anajisikiaje? Au wewe ni mke au mume halafu mnapeana siri zenu labda za magonjwa au madhaifu yenu-labda mume wako kiungo flani hakifanyi tena kazi au mume wako au mke wako anakojoaga kitandani au ana kidonda sehemu fulani-wewe unakwenda kumtangaza na anashindwa hata kutembea ndani ya jamii! Jamani huyu mtu anajisikiaje unamuumiza vipi jamani.

Yesu anazidi kuliiweka tumaini lake kwa Mungu na yeye atashinda. Na fikiria hawa watu uliowasaliti wakimlilia Mungu utapona? Hivyo, tunapotafakari masomo haya ya Yesu kusalitiwa na kupangiwa mipango ya siri, na sisi tuache kuwapangia mipango ya siri wenzetu hasa wale wanao tutegemea-hasa wale watu wa ndoa jamani-tuwe makini. Acheni kusema siri zenu. Ni kuabishana na ni dhambi kubwa ajabu. Ni kuua mtu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni