Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Machi 26, 2020

Alhamisi, Marchi 26, 2020.
Juma la 4 la Kwaresima

Kut 32: 7-14;
Zab 106: 19-23;
Yn 5: 31-47.

SALA ZINATUBADILI, TUNAKUWA VYOMBO VYA HURUMA YA MUNGU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Tafakari ya neno la Bwana leo ianze kwa kuliangalia somo la Injili ambapo tunakutana na Yesu akiwaeleza Wayahudi na viongozi wao juu ya mamlaka yake. Jana aliwaeleza juu ya mamlaka aliyonayo juu ya kuhukumu wanadamu na kuwapatia wafu uzima. Alisema kwamba mamlaka yake ni ya juu-juu zaidi ya nabii yoyote kwani yeye kaungana na Baba na anao upendeleo wa kufahamu chochote kinachofanywa na Baba.

Katika injili ya leo, Wayahudi hawakumuamini, wanaona kwamba anamkufuru Mungu kwani anajikweza mno; yeye ni binadamu tu na si Mungu. Yesu leo anawajibu na kuwaambia kwamba mamlaka aliyonayo haihitaji ushuhuda toka kwa wanadamu ili iwe halali. Anasema kwamba kazi anazozifanya zinamshuhudia kwamba yeye katumwa na Baba; hata maandiko matakatifu nayo humshuhudia. Lakini wao wanakataa kuja kwake na kushindwa kumuamini na kupewa mwongozo na kupata uzima kwa sababu ya ukaidi wao tu. Wao wamejawa na ubaguzi, huwachagua watu wa kuwasikiliza, wanaowaambia ukweli hawawataki kuwasikia na hutumia nguvu kuwarudisha nyuma.

Ndugu zangu, kwa kusema hivi Yesu anazidi kuchoma mioyo ya viongozi wa Kiyahudi na Injili tutakayosikia kila siku ni kwamba wao watapanga mipango ya kumuua-hadi ile siku ya ijumaa atakapoamua kujitoa kwao. Injili hii inatupa moyo kwamba Yesu amekwishakaza moyo wake kutukomboa sisi. Basi, nasi tusiwe kama Wayahudi. Tukubali ukweli tuambiwao na wenzetu hata kama ni mzito, kingine tusichague watu wa kuwasikiliza na kudharau wengine-namna hii hatutaweza kukua kiroho.

Katika somo la kwanza, wana wa Israeli wanamkosea Mungu kwa kutenda kosa kubwa na la kufuru. Wanakimbilia kujenga sanamu na kumkataa Mungu aliyewakomboa katika nchi ya Misri. Hii ni aibu kubwa kwani Mungu katukanwa hadharani mno: yaani alikuwa ndo kawaokoa muda sio mrefu, ndio amewapa chakula, yuko nao katika wingu la moto nao wakamkufuru hadharani, mbele ya macho ya Mungu.

Nasi tuepuke dhambi za namna hii.Tuepuke kutenda dhambi hasa zile za hadharani-makuhani na watumishi wa Mungu tunapotenda dhambi-tujue kwamba tunamtukana Mungu hadharani. Wagonjwa-walioponywa kimiujizaa na watu waliokolewa katika majanga mbalimbali kama ajali lazima watambue kwamba kurudia kutenda dhambi ni kama wanaamua kufanana na hawa wana wa Israeli walioamua kuchonga sanamu. Kutukana matusi mbele za watu huku umevaa rozari, au msalaba ni kumfanya Mungu adharaulike.Tunachotakiwa kufanya ni kuwa na Imani na kumfanya Mungu atukuzwe mioyoni mwetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni