Ijumaa, Machi 27, 2020
Ijumaa, Machi, 27, 2020,
Juma la 4 la Kwaresima
Hek 2: 1, 12-22;
Zab 34: 17-21, 23;
Yn 7: 1-2, 10, 25-30.
KUWEKWA MAJARIBUNI
Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu. Leo tafakari ya neno la Bwana inaanza kwa kuiangalia injili yetu ambapo tunaona kwamba hali ya kutokuelewana kati ya Yesu na baadhi ya viongozi wa Kiyahudi inazidi kuongezeka na mipango ya kutaka kumwangamiza kwa sababu ya matendo na maneno yake yanayotetea mpango wa Mungu unazidi kupamba moto.
Leo inabidi akimbie Yudea kuepuka kumwua na anaporudi Yudea tena anaenda kwa siri kwani wale viongozi wanamtafuta wamwue. Tunachogundua ni kwamba viongozi wa Kiyahudi wameshindwa kuvumilia mafundisho ya Yesu na wanachoamua ni kutaka kumwangamiza, wanamwangamiza mtu mwema ili wao wabakie bila bugudha.
Somo la kwanza linatuambia kwamba mtu mwema hutafutwa kuangamizwa na wabaya kwa sababu uwepo wa mtu mwema unawafanya wao waonekane kama makapi-kwa sababu anawapatia changamoto-unawafanya wadharaulike, waonekane wao kuwa si kitu kwani mtu mwema hupokea sifa zao. Hivyo hutafuta kumwangamiza.
Hivi ndivyo mpango wa shetani ulivyo-shetani anataka kusiwepo na mtu mwema atakayewapatia watu changamoto au mwongozo. Na ndivyo jamii yetu ilivyo-kuna tabia za kutokuwapenda watu waaminifu, wakati mwingine tunawazushia kesi ili wapoteze ushawishi wao katika jamii-watu wakisikia labda unao wafuasi, utaandikwa katika magazeti vibaya, utazushiwa "scandals" lakini mwisho wa siku tutambue kwamba lengo la hawa ni kuipotosha jamii ili sote tupotee kwa kukosa mwongozo. Lakini nakwambia bila watu wema, dunia isingekuwako, bila akina Mt. Francisko, bila akina Padre Pio au watu kama akina Musa kwa taifa la Israeli hakika nakwambia labda dunia ingalikwisha angamia.
Sisi ndugu zangu tuwapende wale watu waliotuzidi kimaadili au kiroho na kisala. Tusiwazushie mambo, tusiongee vibaya juu yao, tukiongea vibaya juu yao ni kwamba ni shetani anatutumia kuiangamiza jamii. Tufurahi kwa uwepo wao kwani wanaisaidia dunia yetu isonge mbele. Tuachane na tabia za kuongea au kusengenya wale watu ambao katika jamii wanajaribu kutetea ukweli. Sikiliza mawaidha ya Mzazi wako, usianze kutangaza dhambi zake kwasababu tu anakueleza ukweli. Ukimtangaza unawakwaza watu na hapa unakuwa msaidizi wa muovu wa kuangamiza ukweli.
Maoni
Ingia utoe maoni