Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Machi 23, 2020

Jumatatu, Machi 23, 2020
Juma la 4 la Kwaresima

Isa 65: 17-21;
Zab 29: 2, 4-6, 11-13;
Yn 4: 43-54.

IMANI KWA YESU

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi hii. Neno la Bwana katika somo la kwanza linatualika tufurahi-kwani kipindi cha furaha kinakaribia, Mungu ataumba mapya, Isaya anasema kwamba Yerusalem hakutakuwa tena kilio, wala vifo vya wachanga. Watu wataishi na kufa katika uzee.

Maneno haya yalisemwa kwa wana wa Israeli waliokuwa wametoka utumwani Babuloni. Hawa walizoea uonevu, na madhulumu makubwa. Waliona kwa macho yao ndugu zao na kaka zao na wazazi na marafiki wakiuawa, na kuteswa vikali na kuuawa. Hivyo kwa kipindi kirefu-uonevu wa namna hii ulikuwa umeshamiri kwa taifa hili. Isaya anawaeleza kwamba hakutakuwa tena na vipindi vya namna hii. Kutakuwako na kipindi cha furaha na amani.

Sisi wengi wetu yawezekana ikawa vigumu kuupokea ujumbe huu wa nabii Isaya-kwa sababu bado tunapigika kutokana na shida na matatizo mbalimbali. Tunasumbuliwa na maumivu ya miili yetu. tuombe Mungu atujalie amani ndani ya vipindi kama hivi. Wengi wetu wanasumbuka, wanaumia, na kukonda katika vipindi vya namna hii. Sisi tunapaswa kuomba amani na utulivu. Bila hivi-hakika tutakosa imani na hata kuikana imani yetu. Wengi kati yetu wamekwishaikana imani yao kwa sababu ya ukosefu wa imani. Tuombe amani ambayo itatupatia utulivu pia.

Kwenye somo la injili, Yesu anamponya mtoto wa Afisa mmoja-afisa huyu alilipokea neno la Yesu kama lilivyo na hivyo likamwezesha mtoto wake kuponya. Yesu hufanya kazi pamoja na wale wenye imani. Tunapokuja kwa Yesu yafaa tumwache Yesu atende. Na tukija kwake, lazima tukubali kushika masharti, fuata muongozo wake. Ndivyo inavyopaswa kuwa hata katika sala zetu, yatupasa kufuata maagizo ya Yesu, tutulie, tumwache Yesu anene. Wengi wetu tumekuwa watu wa kukimbiza mambo, ibada zetu hatumtaki Yesu anene, tunataka ziende haraka-namna hii tunamzuia Yesu kunena-tunajizuia kumsikiliza Yesu-kama alivyofanya huyu Afisa.

Yesu anapaswa kusikilizwa. Tumpatie nafasi. Wengi wetu tumekosa mengi kwa sababu ya kutokumsikiliza Yesu, tumetaka mambo ya haraka haraka. Tumwachie Yesu azungumze. Na kwa namna hii tutaweza kubadilishwa. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni