Jumamosi, Machi 21, 2020
Marchi 21, 2020.
JUMAMOSI, NUMA LA 3 LA KWARESIMA
Somo la 1: Hos 6:1-6 Mungu anawaambia watu wake wamrudie: “Ni upendo anahitaji sio sadaka, na elimu ya Mungu kuliko sadaka ya kuteketezwa”.
Wimbo wa katikati: Zab51: 3-4, 18-21 Ninachohitaji ni upendo sio sadaka.
Injili: Lk 18: 9-14 Luka analinganisha haki ya kujitakia ya Mafarisayo na unyenyekevu wa watu waliomfuata Yesu, waliojitambua kuwa ni wadhambi wanaohitaji huruma.
SALA NI KUJIONA MWENYEWE KWA NJIA YA JICHO LA MUNGU
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari ya neno la Bwana tuaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na nabii Hosea akiongea katika unyofu mkubwa. Anawaambia wana wa Yuda kwamba cha kufanya ni kumrudia tu Bwana-yeye ndiye atakayetuokoa tu. Tusimtegemee mwingine. Twende kwake, atatuadhibu lakini mwishowe hatatuacha. Atatufanya tuteseke, tuonje mateso, lakini anasema kwamba mwishowe hatatuacha kabisa kwani yeye akikuadhibu hakika hakuachagi uangamie, huwa anakujaga na kukuokoa tu-hii ndio faida ya kutembea na Bwana. Unapigika lakini mwisho kuna furaha.
Katika somo la Injili, yule mtoza ushuru anayekuja leo kusali anakuja na mtazamo kama huu wa Hosea katika somo la kwanza. Yeye anakuja ili apigike na Bwana, ili aanguke mikononi mwa Bwana akijua kwamba Bwana ingawa atamuadhibu, mwishowe hatamuacha. Yule Mfarisayo anakuja sio kwa lengo la kujiangusha mikononi mwa Bwana ili apigike na Bwana lakini yeye lengo lake ni kujiunga na Bwana ili awe msaada kwake wa kumsaidia yeye awapige wengine-anawachongea wengine kwa Mungu ili wapigike, yeye anamwambia Bwana kwamba mimi nina ufahamu Zaidi wa watu watenda dhambi-hivyo anawataja ili waadhibiwe na yeye asifiwe. Kwa sababu huyu Mfarisayo alionyesha roho mbaya namna hii, Bwana anamwambia kwamba hakika sitakukaribisha ujiunge nami na kuwataja wenye dhambi. Wewe mwenyewe unamatatizo yako.
Ndugu zangu, somo hili linatoa ujumbe mzito kwetu hasa wale tunaojiona kwamba ni wataalamu wa kusali kiasi cha kufikiri kwamba Mungu amekuwa kama rafiki au ndugu yangu tu. Hii ni dalili mbaya na ya majivuno. Tutambue kwamba Mungu hazoeleki na sala haizoeleki. Sala lazima itufanye tuuone utakatifu wa Mungu na kutambua Zaidi mapungufu yetu. Sala ni kujiangusha miguuni kwa Mungu na kumwambia Mungu afanye kitu. Tusiwaseme wenzetu katika sala au kuwaombea mabaya; hii sio sala. Sala zetu nyingi zinapotea bila kufika kwa Mungu kwa sababu tunatumia sala kama sehemu ya kusengenya wengine, kumsengenya mwingine kwa Mungu, kama sehemu ya kuwaombea wengine mabaya. Mwisho wa siku tunashindwa kumweleza Mungu madhaifu yetu na mahitaji yetu ya kila siku na kurudi nyumbani bila kubarikiwa kama huyu mfarisayo alivyorudi nyumbani bila kitu. Hivyo, ndugu zangu, kila tutumiapo muda wetu wa sala, tuutumie vizuri, tusali vyema, na tumweleze Mungu mahitaji yetu ikiwa ni pamoja na kuuona na kukiri udhaifu wetu . Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni