Alhamisi, Machi 19, 2020
Alhamisi, Machi 19, 2020.
Juma la 3 la Kwaresima
Sherehe ya Mt. Yosefu, Mume wa Bikira Maria.
2Sam 7:4-5,12-14,16;
Zab 89:2-5,27,29;
Rum 4:13,16-18,22;
Mt 1:16,18-21,24 au Lk 2:41-51
Mt. YOSEFU: MTU WA NDOTO NA MTU WA KAZI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu tunapoadhimisha sherehe ya Mtakatifu Yosefu mume wa Bikira Maria. Huyu ni mtakatifu ambaye kwa kweli tumwite mstaarabu, yeye huonekana kama mtakatifu aliyekuwa mkimya, mpole na mwenye kufikiri sana kabla ya kutenda. Tabia hizi zilimfanya aweze kukabidhiwa na Mungu Mama Maria ili amtunze na awe Baba mlishi wa Yesu. Katika kumtunza huku, huyu Yosefu hakulala hata mara moja na Mama Maria, hakukutana naye kimwili hata siku moja; Yosefu alimlinda, akampatia mahitaji yake na kumlinda yule mtoto aliyezaliwa hadi wakati wa Yosefu alipopata kufariki kwake na kuiacha ile familia yake. Kutokana na tabia hizi na utayari huu, Yosefu huitwa mlinzi wa familia na pia nyumba zote za misioni mlinzi wake ni Yosefu; jinsi alivyoweza kumlinda Mama Bikira na ubikira wake hadi kuondoka duniani kama bikira-ndivyo hivyo na nyumba zote za kitawa humwona mtakatifu huyu kama mlinzi wao ili nao kwa maombezi na ulinzi wake waweze kufaulu katika usafi wa moyo na mahitaji yao ya kila siku kama Yosefu alivyompatia Bikira Maria.
Hii ndio sherehe yetu ndugu zangu tunayoiadhimisha na masomo yetu ya leo yanatuelekeza vizuri kabisa katika kutafakari sherehe hii na mtakatifu huyu. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha pili cha Samwel ambapo Mungu kupitia nabii Nathani anaahidi kuusimika ufalme wa Daudi milele kwa kumpatia mtoto atayekirithi kiti chake na huyu mtoto ndiye ambaye pia angemjengea Mungu hekalu. Maneno ya nabii yalimhusu mtoto aliyeitwa Solomoni ambaye angezaliwa na Daudi na yeye ndiye aliyemjengea hekalu Mungu. Lakini unabii ya kwamba hakika ufalme wa Daudi utaimarishwa milele ulikuja kutimia kwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo aliyekuwa mzao wa Daudi ambaye yeye amebakia kuwa mfalme milele na hivyo kuusimika ule ufalme wa Daudi milele. Katika injili, mtakatifu Yosefu alitoa mchango mkubwa sana kuhakikisha kwamba mfalme huyu analindwa na kukua na kuongezeka kimwili hapa duniani. Aliweza kumwokoa na ile jamii ya Kiyahudi ambayo kama Yosefu angewaambia kwamba yule mtoto si wa kwake, hakika Mama na mtoto wangeuawa. Yosefu hakuwa na papara na hivyo aliweza kumwokoa Mama na Mtoto.
Hapa tunayomengi ya kujifunza: wengi kati yetu tunapoteza Baraka ya Mungu kwa sababu tunakwenda papara. Yosefu angekwenda papara, hakika angepoteza hii ngekewa ya yeye kuja kuwa mlinzi na mlishi wa Masiha. Sisi kwa sababu ya kwenda haraka haraka, tumeishia kutupa watoto au hata kukataa watoto wa mashangazi au wajomba au waliokotwa wakiletwa nyumbani mwetu. Nakwambia kuna waliokataa watoto fulani wasiletwe nyumbani kwao wakiwa wadogo-lakini sasa wanaposikia kwamba wale watoto ni matajiri wanakwenda ati na kusema mimi aise nataka sasa uje kwangu. Kuna kina baba walikataaga watoto wakapelekewa baba wengine au wakapelekwa vituoni vya watoto. Sasa wale watoto wamefanikiwa ajabu; ni wanamuziki na matajiri wakubwa na baba zao wanajitokeza ni mimi-na watoto wanawakataa-tuache ubinafsi, tusikatae watoto. Au kwa sisi tunaotoaga mimba-baadhi ya watoto tuliowatoa nakwambia labda sasa hivi ungekuta ni mainjinia na maprofesa wakubwa-tunapoteza mengi kwa sabbu ya ubinafsi.
Kingine tujifunzacho ndugu zangu ni kuhusu ushauri toka vijiweni. Yosefu angekwenda kijiweni asingeweza kuishi na Maria au kumpokea. Na sisi tuangalie sisi tunachukuaga ushauri vijiweni au kwenye mabaa halafu ndio unaona kwamba ati ndio umepata ushauri safi-yaani ushauri toka kwa mlevi mwenzako? Angalieni, vijiwe vinaua ndoa zetu. Watu wanafukuza wake na watoto kutokana na ushauri wa vijiweni. Kina mama wanakimbia waume zao kutokana na ushauri wa vijiweni.
Kingine tuwe walinzi jamani. Ukiona mtu maskini aidha binti anayetafuta ada au kazi kwako halafu anakuja kwako kuomba kazi akitegemea ulinzi na huruma yako mhurumie. Kuwa mlinzi kwake, usitumie shida zake kummaliza. Hii ni dhambi kubwa ajabu. Unamwajiri na hapo hapo unamtaka kimapenzi-Kuwa Yosefu. Tunahitaji akina Yosefu hapa jamaniwalinde uhai wao.
Tunahitaji kina Yosefu wapya katika familia zetu. Watu wasio wavumilivu, kina baba ni ubabe tu, wanawake kibao, nyumba ndogo kila mahali, kila siku baba anakuja na kuwambia watoto pale kuna mdogo wenu, mara hapo, mara kule, mara pale juu pale, (wewe umekuwa jogoo?) watoto hawapatiwi mahitaji yao, yote hayo ni mambo yanayotufanya tuhitaji akina Yosefu. Tuwe watu wa imani kama somo la pili linavyosema ili ahadi ya Mungu iweze kutimizwa katika maisha yetu kama Yosefu.
Maoni
Ingia utoe maoni