Ijumaa, Machi 13, 2020
Ijumaa, Machi 13, 2020,
Juma la 2 la Kwaresima
Mwa 37:3-4, 12-13, 17-28;
Zab 105:16-21;
Mt 21:33-43, 45-46
UPENDO UNAOTESEKA
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana tuanze kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na habari za mtoto wa Yakobo jina lake Yusufu. Huyu alipendwa sana na baba yake, naye alikuwa bado anao umri mdogo, akili yake ikiwa aminifu kabisa, alikuwa ana imani yote kwa ndugu na wazazi wake kwani alijijua kwamba ni mdogo na alihitaji miongozo yao. Hivyo, kalikuwa kama katoto kakionyesha uaminifu wote kwa kila ndugu zake; alikuwa kalelewa katika mazingira ya kupendwa, alikuwa hajazoea kuona mtu akimchukia. Sasa leo Baba yao anamtuma aende kuwajulia hali ndugu zao, naye anafika kwao, anawaona, anafurahi kukutana nao na anajiaminisha kwao. Bila shaka alishangaa kuona kwamba wanamchukia na kutaka kumtenda uovu huu. Bila shaka aliumia sana-kwa sababu yeye alikuwa ni mtoto aliyezoea kupendwa karibu siku zote. Naamini aliwaangalia kwa huruma sana na uchungu ndugu zake walipomkamata na kumtupa katika kile kisima ili afe ndani. Ebu jiulize haya macho ya huyu kijana yaliwaangalia vipi wale ndugu zake? Ebu jiulize uchungu alioupata? Jamani jamani? Kweli mtoto huyu alikwazika sana kuona kwamba ndugu zake wameamua kumtenda kama mgeni, jamani.
Hizi habari zanikumbusha habari za Mama anayemtoa mimba mtoto wake au mama anayeamua kumtupa mtoto wake jalalani. Jiulize uchungu yule mtoto anaoupata jamani, huwa anakuangalia vipi? Mtu aliyekutegemea utunze uhai wake unageuka kumuua? Jamani? Hakika huyu mtoto hukwazika sana. Au unakuta ndugu wamezaliwa pamoja halafu hawaongei au unashangaa ndugu mmoja anakuja na kumtendea mwenzake uovu au anakula njama na wageni dhidi ya ndugu yake-jiulize ule uchungu yule ndugu yake anaoupataga? Au wewe mke ulaye njama kumwangamiza mume wako-unajua uchungu anaoupata akiona unafanye hivyo? Yaani mtu aliyekutegemea unamtenda hivyo? Naamini huwa anapata uchungu wa kutaka kufa. Ndugu zangu, somo hili litufanye tutambue uchungu uliopo ndugu mtendeanapo uovu au umsalitipo rafiki yako.
Katika somo la Injili tunasikia habari za viongozi wa taifa la Israel wanaoelezwa kama wapanga shamba waliokuwa waovu sana. Walipomuona mtoto katumwa waliamua kumteketeza ili wachukue urithi wao wakitegemea kupata faida kumbe ikawa ndio kinyume-kwani yule Baba alikuwa na nguvu za ziada, alikuwa hafi kama walivyokuwa wanadhania ili wapate urithi. Haya ni mambo yanayotendeka ndani ya jumuiya yetu. Wapo watu wajiingizao katika vitendo vya wizi. Na ili kupoteza ushahidi, wanauwa watu wote, hata wale wasio na hatia ili kuua ushahidi wasije wakatoa siri. Huu ndio uovu ulivyo, ni uovu mbaya. Bwana akija hakika atafanya adhabu kama ya hawa Waisraeli. Yesu ni mkuu ana macho ya moto (Ufu 19:12)-maana yake anaona kila kitu kinachotendeka hata kama iwe ni dhambi uliofanya kwa siri namna gahani. Na tusipowakemea na sisi tutateseka kwa kuadhibiwa kwao kwani kama ni ndugu yako basi kwa namna moja itabidi uteseke.
Maoni
Ingia utoe maoni