Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Machi 14, 2020

Jumamosi, Machi 14, 2020,
Juma la 2 la Kwaresima

Mika 7:14-15,18-20;
Zab 103;1-4, 9-12;
Lk 15: 1-3, 11-32

KUMRUDIA MUNGU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo tutaanza kwa kuliangalia somo la Injili ambapo tunakutana na simulizi la mwana mpotevu. Huyu alingangania sehemu yake ya urithi kwa nguvu, akachukua mali zake na kwenda kula na makahaba, alimwonesha baba yake tabia mbaya na dharau na kumlazimisha ampe urithi. Halafu mwishowe mambo yanakuwa magumu na kuanza kurudi na Baba anampokea. Simulizi hili nalifananisha na hali ya sasa iwakumbayo hasa vijana wengi-unakuta kijana awe wa kike au wa kiume inafika muda fulani, hasikilizi maongozi ya baba yake, anajidai kuwa na akili kupita kiasi, anatukana hata wazazi wake, hataki hata kusikia mwongozo wao. Lakini mambo yanakuwa magumu unashangaa anarudi tena kwa wazazi wake, upole umemjaa kabisa, majivuno yote kwisha na ndio anamtegemea mama yake ampatie kitu. Hili ni jambo linalotokea-na mzazi anakupokea baada ya kumwonyesha hivyo majivuno yako. Tumshukuru Mungu kwa upendo tunaooneshwa na wazazi wetu hawa.

Hapa tujifunze kitu ndugu zangu: kwanza vijana tuache kujiona kana kwamba sisi ni wajanja kuliko wazazi wetu, tuache kufikiri kwamba tunayajua maisha kuliko wazazi wetu, au kufikiri kwamba tunajua kuyafurahia maisha kuliko wazazi wetu-wao wameishi miaka mingi na wameona mengi. Tusifikiri kwamba ati wamepitwa na wakati-wakikuambia kitu waweza kuona kama cha kijinga lakini fikiria mara mbili. Kila siku wazazi wetu wanatusamehe kama Baba wa mwana mpotevu.

Yesu anatumia mfano huu kufundisha kwamba upendo wa Mungu alionao kwetu ni zaidi hata ya upendo wa mzazi kwa mtoto-yeye atupenda Zaidi. Somo hili limewekwa kipindi hiki cha kwaresima ili litufikirishe namna jinsi kila mmoja wetu alivyowahi kuwa mwana mpotevu mbele ya Mungu, namna kila mmoja wetu alivyoweza kutumia mali, uwezo wake, viungo vyake alivyopewa na Mungu kwa kumkufuru Mungu. Mfano, ni pale viungo vyetu vya uzazi vinavyopevuka-na mara moja tunasema sasa vitumike kwa uzinzi, tunasema sasa ni wakati wa kuvifurahia-hapa ni kuwa kama mwana mpotevu-hii ni kwa sababu tuliviona vikiwa vidogo, havina kitu, sasa vimechanua tunajivuna, tunaruka navyo na wakati utafika ambapo vitaishiwa nguvu kabisa na kuvirudisha kwa baba tukiomba msamaha. Somo hili litufanye sisi vijana tuache kutapanya urithi wa viungo tulivyonavyo kwa ajili ya uzinzi.

Somo la kwanza nabii Mika atueleza zaidi juu ya upendo na huruma ya Mungu kwetu sisi. Nasi tuzidi kumrudia Bwana katika kwaresma hii na kumwomba msamaha hasa kwa kuvitumia viungo vyetu vibaya. Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni