Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Machi 11, 2020

Jumatano, Marchi 11, 2020.
Juma la 2 la Kwaresima

Yer 18:18-20;
Zab 31:5-6,14-16;
Mt 20:17-28.

JE, TWAWEZA KUKINYWEA KIKOMBE CHA YESU?

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Tafakari ya neno la Bwana katika asubuhi ya leo tuanze kwa kuiangalia zaburi ya wimbo wa katikati ambapo tunakutana na mzaburi anayelia akimuomba Mungu amuepushe na maadui wake wakali wanaotaka kumshambulia. Maadui hawa ni mashuhuri na wenye nguvu na wamedhamiria kumshambulia huyu muumini. Lakini yeye ameyaweka matumaini yake yote kwa Mungu na anamuomba Mungu amuonyeshe njia aweze kukabiliana na maadui hawa. Sala hii ya mzaburi inafanana moja kwa moja na ya Yeremia tunayoisikia katika somo la kwanza leo. Katika somo hili, Yeremia anatafutwa auawe na mbaya zaidi wanaotaka kumuua ni watu wa nyumbani mwake-wale aliowategemea kwamba wangemlinda-watu wa nyumbani mwake wamegeuka na kuanza kumshambulia. Kilichomfanya Yeremia ashambuliwe namna hii ni kwa sababu yeye alibakia mwaminifu katika kuutangaza unabii alioambiwa autoe kwa watu. Unabii alioambiwa na Mungu kwamba autoe ndugu zangu ulikuwa mgumu sana-yeye alitumwa awaambie watu kwamba wasijaribu kumpinga Nebuchadneza mfalme wa Babuloni. Mungu alimtuma awaambie watu kwamba wajiweke chini ya mfalme huyu, yeye amemruhusu mfalme huyu kuja kuwatawala kutokana na dhambi zao. Watu hawakuwa tayari kupokea hili. Walimkamata Yeremia na kumpatia kipigo cha hatari. Walimuona kana kwamba ni msaliti wa taifa, hata ndugu zake walikuwa tayari kupanga wamuue. Lakini Yeremia alizidi kuwaambia jamani huu ujumbe sio wangu-ni Mungu mwenyewe amesema-mimi nimeambiwa niwatangazie tu, sasa mbona hamuupokei? Lakini hakueleweka-na kwa kweli Yeremia alipigwa sana. Hakuna nabii aliyewahi kupata mateso kama Yeremia. Na katika mateso yake alijaribu hata kuwakimbilia watu wa nyumbani mwake lakini nao walimtenga na kutaka kumuua. Hivyo alizidi kumlilia Bwana na kwa kweli Bwana alimuokoa na wale watu. Mfalme Nebuchadneza alikuja Yerusalemu, akauteketeza ule mji, na wale waliompiga Yeremia waliuawa na wengine kufanywa viwete na wengine kupelekwa utumwani.

Somo hili ni nguvu yetu hata wale ambao tunaongea kati ya watu wasiotusikiliza. Ama kweli kama kitu ni cha ukweli na wanakikataa, basi muda utaamua. Sisi tubakie katika ukweli.

Katika somo la Injili twawakuta Mama wa wana wa Zebedayo akiwaombea wana wake nafasi nzuri. Yeye anaomba kama mama anayetaka watoto wake wawe na sehemu nzuri-jambo ambalo kila mama angependa mtoto wake afanyiwe hivyo. Lakini Yesu anatumia nafasi kufundisha kwamba nafasi ambayo kila mtu anapaswa kuitafuta ni utumishi-sio maisha ya kuwakalia wengine. Kama Yesu naye angekuja kungangania maisha ya kuwakalia wengine, hakika ujio wake ungekuwa bure tu. Sasa angekuwa ndio amekuja kufanya nini sasa? Yaani angeingizwa kwenye hali moja na akina Sadamu Huseni, Idi Amin, na Adolf Hitler-na kama ni hivyo ungekuta hakuna anayejaribu kumfuata. Lakini yeye katuletea kitu tofauti na ndio maana tunajaribu kumfuata. Nasi ndugu zangu tutambue kwamba kama nasi tutangangania maisha ya kuwakalia wengine, tujue kwamba hatuna cha ziada tutakachoweza kusema kwamba tutaiachia hii dunia. Na tayari dunia imeshakuwa na watu hodari katika kuwakalia wengine. Kuna akina Sadamu na Hitler, wote hao-unafikiri waweza kuwashinda? Lakini kama tutachagua maisha ya kuwatumikia wengine, basi wengi watavutwa kwetu na tutakuwa na cha kujivunia katika maisha yetu kama tunavyojivunia watakatifu siku hizi. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni

Thomas wafula

Tumshukuru mwenyezi Mungu

Ingia utoe maoni