Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Machi 09, 2020

Jumatatu, Marchi 9 , 2020
Juma la 2 la Kwaresima

Dan 9:4-10
Zab 79:8-11,13
Lk 6:36-38

USIHUKUMU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana itaanza kwa kuiangalia zaburi ya wimbo wetu wa katikati ambapo tunamkuta mzaburi akimuomba Mungu msamaha na kumwambia Mungu asimtende kadiri ya matendo yake-yaani katika hukumu zake azidishe huruma zaidi na zaidi, kwani endapo Mungu hataonyesha hili, basi mzaburi anamwambia kwamba mimi nitaishia kuangamia na sitaweza kufika kwako kabisa. Yule mtoza ushuru alipoenda kusali kanisani alitumia maneno ya mfano huu na kubarikiwa sana. Hata Daudi mwenyewe alitumia katika sala zake sala ya mfano huu na kuishia katika kubarikiwa. Lakini wote waliotumia mfumo tofauti wa sala mbele ya Mungu waliishia kujivuna mbele ya Mungu.

Katika somo la kwanza, tunakutana na nabii Danieli akitambua ukweli wa maneno haya na yeye katika sala yake leo kuliombea taifa la Israeli yeye anasali kwa kumuomba Mungu msamaha ili asije akahukumu bila huruma. Wanaona kwamba kwa Mungu kinachohitajika ni huruma na endapo utakwenda mbele ya Mungu kwa moyo wa majuto, tutaishia kubarikiwa. Yeye alitambua kwamba katika historia ya taifa la Israeli, ni yule tu amjongeaye Mungu kwa moyo mnyenyekevu akimuomba msamaha hubarikiwa.

Katika injili, Yesu sasa anatuambia kwamba kwa sababu Mungu ni mwenye huruma na yeyote anayekwenda kwake kwa moyo mnyenyekevu akitafuta huruma hupata, sasa anasisitiza kwamba nasi lazima kumuiga Mungu-lazima kuwa watu wa huruma na na sisi kwani Baba yetu ni mwenye huruma-kama wewe unataka Mungu akusamehe, basi na wewe lazima uwe tayari kuwasamehe wengine.

Ujumbe huu ni mzito hasa kwetu sisi tulio na roho ngumu ya kusamehe na kuweka visasi-pia maneno haya ni mazito kwetu sisi ambao huwa tunakasumba ya kudai watu hadi senti ya mwisho. Hukubali kumwachia mwenzako senti ya deni lako-kumbuka ndugu zangu yote uliyonayo umepewa. Na zaidi wakuta umejaliwa vingi na katika uhalisia unachodai hata ukikosa huwezi pungukiwa kitu, unaona mtu anateseka na familia kuwapa watoto chakula, wewe unamdai kwa nguvu pengine fedha zako ili ukanywe pombe au kufanya kitu ambacho unajua ukikosa huwezi dhurika. Hivyo, hata katika kudai mwenzako deni, tuweke huruma ndani yake pia. Katika hiki kipindi cha kwaresma tusamehe hata wadeni wetu jamani. Tunataka Yesu atusamehe dhambi zetu lakini hatukubali kusamehe wenzetu madeni yetu hata pamoja wana hali mbaya kuliko sisi. Tusamehe Madeni, ni haki yako lakini tambua haki iliochanganyika na huruma ndani yake ni tabia ya Kimungu.

Maoni


Ingia utoe maoni