Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Machi 06, 2020

Ijumaa, Marchi 6, 2020,
Juma la 1 la Kwaresima

Eze 18:21-28;
Zab 130: 1-8;
Mt 5:20-26.

KUWA MWEMA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunamkuta nabii Ezekiel akituambia kwamba sio Mpango wa Mungu kufurahia kufa kwa mtu mwovu bali auache mwenendo wake. Hivyo anasema muovu atakayeacha njia yake na kugeuka, huyo ataponywa na Mungu lakini Mchamungu atakayeiacha njia yake njema na kuasi atakufa katika uovu wake-asitegemee kwamba ule wema alioutenda mwanzoni utamuokoa.

Hili ni fundisho kubwa sana hasa kwa baadhi yetu ndugu zangu. Kuna baadhi yetu tunafikiri kwamba wakati fulani nilisali sana. Sasa siendi hata kanisani nikijifariji kwamba zile misa nilizozienda zitaniokoa. Au unakuta baadhi yetu hatuungami na tunasema nikiwa mdogo niliungama sana, sasa ngoja nitende dhambi kidogo, ni wakati wa kulipia madhambi. Au wakati mwingine nasema naenda hija mwaka huu na kusali labda kwa siku tisa halafu kwa kipichi chote cha mwaka sisali tena. Huku ni kupotoka ndugu zangu na namna hii hatutaweza kumfikia Mungu. Kama ni wema tuwe wema siku zote. Unapoamua kuwa mwema kwa Mungu, hatuweki masharti. Unakuwa mwema tangu mwanzo hadi mwisho, usije ukampangia Mungu na kumwambia kwamba aa, Mungu nilikutii sana pale mwanzoni, acha sasa nitende dhambi, nipe kapozi kadogo-namna hii siyo. Mungu apenda kitu kikamilifu, na sisi tumpatie kitu kikamilifu. Kama kweli tumeamua kumtii, basi tumtii siku zote, tubakie katika muungano naye, sio siku moja nasema-aa, leo natenda kadhambi kadogo bwana=hapa hatujampenda Mungu, hapa bado tutakuwa tunamkosea Mungu. Tulio na tabia hizi tuache. Tunaosemaga-ati leo ni sikukuu, ngoja nilewe kidogo-sio namna nzuri. Kwa Mungu hakuna siku iliyo ya mlegezo legezo.

Injili tunamkuta Yesu akiendeleza mada hii kwamba uaminifu ni kubakia katika muunganiko na Bwana siku zote. Sio kulegeza legeza. Yeye anawaambia kwamba wale wafarisayo walikuwa na hali ya kulegeza legeza uzito wa amri za Mungu. mfano, unakuta Mfarisayo anapeleka sadaka hekaluni halafu kumbe hajapatana na ndugu yake, Mfarisayo anajidai kutamka amri ya tano ya Mungu usiue na kumbe moyoni anakuangalia kwa hasira. Yesu anawaeleza wanafunzi wake kwamba wasiige mfano kama huu kwa sababu wao walikuwa hawafanyi kitu kikamilifu mpaka mwisho. Yesu anawaeleza kwamba kama mtu anakubaliana na amri ya Mungu kwamba usiue, basi ajue kwamba amri hii inakupasa umpende jirani yako kuliko vyote-hata kumwangalia vibaya usimwangalie. Usimseme. Huku ndiko kuishika amri. Yeye anashangaa kuona wafarisayo wanasema usiue lakini bado wanachuki na watu moyoni. Ndio maana yesu anawaambia wanafunzi wake haki yao iwazidi ya wafarisayo-yaaani kama ni kutimiza sheria za Mungu-wasiweke kamlegezo hata siku moja.

Somo hili ndugu zangu ni funzo kwetu sisi ambao mara nyingi tayari tumeshaandaa namna za kujitetea na kufanya na kuhalalisha ili kutenda dhambi. Mwingine anasema nafanya maramoja tu sitarudia! Hii mara moja sio dhambi? Anayempenda Mungu hatarusuhu kutenda dhambi hata mara moja. Unakuta mtu anasema-nalewa tu kwa leo, hakuna kitu kama hicho-mpende Mungu siku zote, unakuta mtu anasema-aah kwa sababu nimetukana au kufanya uzinzi kwa mara ya kwanza sio dhambi-hakuna kitu kama hicho. Vyote ni dhambi. Dhambi haina cha ya kwanza na ya mwisho. Zote ni hatari. Hali ya kusema dhambi za mara ya kwanza sio dhambi au sio nzito tuache-tuogope dhambi kila wakati.

Maoni


Ingia utoe maoni