Jumatano, Machi 04, 2020
Jumatano, Marchi,4, 2020.
Juma la 1 la Kwaresima
Yon 3:1-10;
Zab 51:3-4,12-13,18-19;
Lk 11:29-32
KUMKUBALI YESU NA UPENDO WAKE!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linatupatia ujumbe muhimu kabisa wa kutuongoza katika kipindi chetu cha Kwaresima. Na neno hili tutaanza kwa kuuangalia wimbo wa katikati ambapo tunakutana na ujumbe kwamba moyo uliovunjika na kupondeka ee Mungu hutaudharau. Hii ni Zaburi aliyoiimba Daudi akiwa katika unyenyekevu mkubwa na hali ya kujiona mnyonge baada ya kutenda kosa la uzinzi na uuaji-kumuua Uriah na kumchukua mkewe. Aliisali katika moyo wa kupondeka na unyenyekevu mkubwa na hii ilimsaidia kupokea msamaha toka kwa Mungu na kubarikiwa tena. Nabii Yona katika somo la kwanza alikuja miaka mia sita baada ya maneno haya kusemwa na Daudi na yeye sasa katika somo la kwanza anawashauri watu wa Ninawi wajivike moyo uliovunjika na kupondeka kama alivyojivika Daudi ili wapate msamaha toka kwa Mungu la sivyo wataangamizwa. Watu wa Ninawi walikubali ujumbe huu na tunasikia kwamba walijivika moyo uliovunjika na kupondeka na mwishowe walihurumiwa. Yesu, katika injili anakuja miaka karibu mia nne baada ya Yona kusema maneno haya kwa watu wa Ninawi na katika Injili Yesu anawaeleza Wafarisayo kwamba hawatapewa ishara nyingine isipokuwa ile ya Yona.-ishara ya Yona ni ishara ya majuto, ishara inayonitaka nijione kwamba mimi ni mkosefu nihitajiye neema ya Mungu, ishara initakayo nikazane niupiganie wokovu wangu, ishara initakayo nijivike moyo wa kuvunjika na kupondeka kama walivyojivika wale watu wa ninawi na kama alivyojivika Daudi na kusamehewa. Walipofanya hivi walipata matunda makubwa maishani mwao lakini Wafarisayo watakapokataa kufanya hivi basi watapatwa na matatizo mengi na kuukosa wokovu maishani mwao.
Mtazamo huu ndugu zangu ndio unaonifaa mimi na wewe kwa kipindi hiki. Lazima niende mbele za Mungu, nikiwa na moyo uliovunjika na kupondeka, moyo wa majuto na kuomba msamaha na kwa namna hii nitaweza kuona nguvu ya Mungu maishani mwangu-na kukifanya kipindi hiki kiwe cha faida kwangu. Tuombe msamaha kwa wale tuliowakosea, tutumie sakramenti ya kitubio vizuri. Dunia inapata shida kubwa kwa sababu watu hatujioni kama wadhambi, tunajiona kwamba ni wema-na dunia inalaaniwa kila siku. Tutakapojiona kwamba sisi ni wadhambi, dunia yetu itabarikiwa tena-familia na jumuiya yangu itabarikiwa tena. Na magomvi yatapungua. Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni