Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Machi 03, 2020

Jumanne, Marchi 3, 2020
Juma la 1 la Kwaresima

Isa 55:10-11;
Zab 34: 4-7, 16-19;
Mt 6: 7-15

KUJIFUNZA KUSAMEHE!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu siku ya leo. Leo neno la Bwana tutaanza kwa kuliangalia somo la Injili ambapo tunakutana na Yesu akitufundisha namna ya kusali. Anatueleza kwamba sala ni tendo takatifu ambalo kwa hilo tunaungana na Mungu. Ndiyo njia tu mwanadamu anaweza kuongea na Mungu. Na njia hii ni muhimu. Wapo watu wengi sana wameitumia na wamefanikiwa vizuri kabisa. Kwa njia ya sala watu kama akina mtakatifu Fransiko wa Assis waliona maono makubwa-watu wamefanya miujiza mikubwa na wamepata miujiza maishani mwao kwa njia ya sala. Kwa kweli hata wewe mwenyewe kuna mahali inafikaga unajiona unafaulu katika baadhi ya mambo-lakini ukijaribu kujiuliza kwa undani utaona kwamba hapa pana mkono wa Mungu. Sio kwa nguvu zangu. Huu ni muujiza. Kila mtu ana stori yake ya kuelezea.

Ndugu zangu, lakini cha ajabu ni kwamba, licha ya ukweli kwamba sala ina nguvu nyingi kiasi hicho, watu wanaichezeaga sala na katika Injili Yesu anasema kwamba watu wanasali kwa kupayuka-bila kutafakari, kwa kujionyesha ili waogopwe na watu na wapewe sifa na watu. Yesu anapinga kuchezea sala namna hii. Yeye anafundisha sala na namna ya kusali na anasema kwamba ukianza kusali-kwanza anza kwa kumtukuza Mungu, yaani unatambua ukuu wake, halafu omba ili aendelee kukubali kuiongoza dunia-aitawale na mapenzi yake yaenee kila mahali na si mapenzi ya muovu. Halafu tumweleze shida zetu hasa juu ya mahitaji yetu kama chakula na kumwomba atusamehe dhambi zetu na asituingize katika majaribu. Sala hii yahitaji tafakari na haina mahali popote inaposisitiza kwamba mtu ajitukuze mwenyewe au atumie sala kwa kutishia watu. Namna hii sala huwa takatifu na Mungu hutusikia.

Katika somo la kwanza, Mungu anasisitza kwamba maneno yake na mipango yake si mchezo. Kila asemacho hatanii na mipango yake na neno lake lazima litekeleze ile kazi iliyotumwa kutekeleza kama mvua iinyeshayo ardhi na ardhi kuchipua. Huu ujumbe twaweza kuutafakari unamaanisha kwamba tujue Mungu ni tofauti na sisi na pale unapotaka kuongea naye au kufanya agano naye au kutaka kusali, jua kwamba unaongea na ngazi ya juu-usifanye mchezo. Kama ni kwenye sala tuwe makini. Kwenye sala unaingia katika mazungumzo na Mungu, unapanga naye mipango, lazima kuwa makini sana tusije tukafikiri kwamba tunapanga mipango ya hivihivi tu.

Masomo yote haya yanatupatia ujumbe mkuu sana kwaresma hii. Yanatuambia juu ya kuheshimu sala. Sala si kujionyesha. Waweza kuja kusali ukaishia kulaaniwa kwani unaishia kwenye kumkufuru Mungu, au kujisifu mwenyewe kama yule Farisayo. Tuwe na mipango-nikija kanisani niwe na nia, nisali-nimpe Mungu utukufu na mimi nipate baraka.

Maoni


Ingia utoe maoni