Ijumaa, Februari 28, 2020
Ijumaa, February 28, 2020,
Ijumaa baada ya Jumatano ya majivu
Isa 58: 1-9;
Zab 51: 3-6, 18-19;
Mk 9: 14-15.
NJAA KWA AJILI YA MUNGU!
Karibuni ndgu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana pia tafakari yetu ya kipindi cha kwaresma kwa siku ya leo tunaanza kwa kukiangalia kitabu cha nabii Isaya ambapo tunamkuta nabii akielezea maana muhimu ya kufunga. Anaeleza kwamba kufunga si kujitenga na matatizo ya mwenzako na kujifikiria wewe. Huwezi kusema kwamba nimefunga halafu hapohapo ukajitenga na matatizo ya wenzako. Mwenzako hawezi kuwa anakufa njaa, anaendelea kudhulumiwa, anaendelea kulipwa mshahara kidogo, anazidi kulala na njaa na mimi nikajisifu ati napita nyuma au mbele ya nyumba yake na kwenda kusali na kufunga. Mungu anasema kwamba kufunga kwa namna hiyo hakupokei. Kufunga anakokupenda ni lazima tukubali kushiriki katika shida za wengine. Ndilo linalotakiwa ndugu zangu.
Ukweli Mungu anatambua faida ya matendo ya kufunga na kusali. Kunakufanya usafiri na Mungu na kuungana naye na Mungu anapenda mtu anayefunga na kusali. Wakina Musa, Daudi na Ester walifunga wakiomba na Mungu aliwasikiliza. Popote pale mwanadamu alipomuomba Mungu kwa kufunga na kusali hajawahi kumtupa. Lakini tatizo ni kwamba matendo haya yalikuja kuchakachuliwa/ Kuharibiwa na viongozi wa kidini ya Kiyahudi. Mfungo ulikuja kuwa kama sehemu ya watu kama Wafarisayo kutishia wengine, kuonekana kuwa ni wema, na kuwa wana madaraka zaidi. Ndivyo mfungo ulivyokuja kuwa. Hivyo, mfungo ulipoteza maana yake na kwa sababu hiyo ukawa hauzalishi matunda mazuri kama ipasavyo. Leo sisi tunaambiwa ndugu zangu kwamba mfungo wangu lazima nianze kwa kuangalia pembeni yangu kuna nini na nani. Usikute naenda kutoa msaada kule nitakapoonekana na vyombo vya habari au kule kuliko na kusifiwa ili wanisifu na kumbe watu pembeni wanakufa. Acha unafiki. Anza na yule wa pembeni yako, yule ambaye hakuna hata chombo cha habari kimoja kitakachokuona.
Katika Injili, Yesu anasistiza kwamba baada ya Bwana harusi kuondolewa, wanafunzi wataanza kufunga. Bwana arusi ni Yesu mwenyewe. Wakiwa na Yesu, wanafunzi hawana haja ya kufunga kwa sababu wako na Bwana. Tunafunga ili tuwe na Bwana. Sasa kama Bwana yupo pamoja nawe, hakuna haja ya kufunga. Lakini Bwana atakapoondolewa, watabidi wafunge ili kumleta Bwana katikati yao. Kweli ndugu zangu hili lilitokea. Mitume kama akina Petro (Mdo10:10) walianza ilibidi wafunge baada ya Bwana kutoka ili waungane naye. Nasi ni mwaliko kwetu ndugu zangu. Tunafunga ili tuwe na Bwana, asafiri nasi akae nasi maishani. Hii iwe sababu yetu sisi kufunga katika kwaresma hii ndugu zangu.
Maoni
Ingia utoe maoni