Ijumaa, Februari 14, 2020
Februari 14, 2020 Ijumaa
JUMA LA 5 LA MWAKA
1Fal 11:29-32;12:19
Zab 81:9-14
Mk 7: 31-37.
EPHATHA, FUNGUKA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunasikia dhahiri juu ya matokeo ya kosa la Solomoni kwa taifa nzima la Israel. Taifa sasa linateseka na linapatwa na mpasuko. Anatokea mfalme mwingine kutawala makabila kumi ya Israel na kwa kipindi chote cha utawala kutakuwa na fujo kati ya wafalme hawa wawili wa Israeli, yaani mfalme wa Yuda na mfalme wa haya makabila kumi ya Israeli. Hasara nyingine itakayotokea ni kwamba hizi falme mbili zitadiriki kuungana na mataifa mengine ili zipigane kati yao wenyewe. Hiyo ndiyo hasara ya dhambi ndugu zangu. Hiyo ndiyo hasara ya mtu mwenye hekima, mtu anayetegemewa anapotenda kosa, anaposhindwa kuishi kama anavyotakiwa-sasa hasara yake huwa hivyo ndugu zangu-hasara kubwa.
Katika somo la injili tunamkuta Yesu akitenda miujiza mikubwa kiasi kwamba hata na watu nao wanafurahi sana kwa hiki kinachotendwa na Yesu. Yesu anakuwa sababu ya watu kufurahi na kubarikiwa. Yote haya ilitokana na ukweli kwamba yeye alizidi kumtii baba na hakukubali kwenda kinyume na mapenzi yake.
Ndugu zangu, haya masomo yetu ni fundisho kwetu. Kuna watu tulioaminiwa, iwe ni viongozi wa dini, baba, mama, au mtu yeyote kati ya jumuiya hata kama ni mkuu mahali fulani. Tujue kwamba kwa utii, kwa hekima, na kwa kumcha Mungu tutafanikiwa kuliongoza kundi katika njia sahihi. Lakini endapo kama tutaishia katika kutokutii na kuliongoza kundi tulilokabidhiwa katika dhambi tujue kwamba tunajiletea hasara kubwa na tunakuwa saababu za wengine kulaaniwa.Hivyo, ndugu zangu leo tujifunze faida ya kuwa waaminfiu. Wengi waliokataa kuwa waaminifu wamekuwa sababu ya wengine kuteseka. Dhambi huleta hasara hata kwa wale wasio na hatia.Tusiwe sababu za wengine kuteseka.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni