Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Februari 11, 2020

FEBRUARI 11, 2020
JUMA LA 5 LA MWAKA

1 Fal 8:22-23.27-30
Zab 84:2-4.9-10
Mk 7: 1-13.

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunamkuta Solomoni bado akiendelea kusali katika hekalu. Na leo anamuomba Bwana akimsihi akubali kukaa ndani ya hilo hekalu kwa sababu ni Mungu mkuu mno. Anajua kwamba hako kahekalu hakawezi kumtosha Mungu kwani hata mbingu zenyewe zilivyokubwa haziwezagi kumtosha Mungu, na hata dunia tunaweza kusema kwamba haiwezi kuwa hata kiti cha kuwekea miguu ya Bwana. Sasa, anamuomba Mungu akubali tu kukaa ndani ya kale kahekalu, na asikilize sala zao sisi wanadamu tunaokwenda kusali hapo.

Ndugu zangu, hapa katika hili somo twagundua mambo muhimu. Kitendo cha hata Yesu, kukubali kukaa katika Ekaristi na kukaa kanisani ni kwa sababu ya upendo tu na ni kwa faida yetu. Yote hayo anayafanya kwa faida yetu. Anakaa pale, halafu wakati mwingine tunamdharau, hatumsujudu, yote haya ni makosa yetu lakini Yesu kasukumwa tu na upendo. Hivyo, tuwe makini na kuweza kuona upendo mkubwa namna hii.

Katika Injili, tunakuta kwamba Wayahudi walishindwa kutafakari na kugundua undani wa pendo kama hili. Wao badala ya kutengeneza sheria za kumshukuru Mungu kwa kukubali kukaa ndani ya hekalu, wao waliona ile kama sehemu ya kujitengenezea mtaji na kujinufaisha. Wanasheria na Mafarisayo wakatengeneza sheria ambazo ziliwafanya wao wanufaike na waheshimiwe zaidi, sheria zilizofanya tamaduni za Kiyahudi ziheshimike Zaidi kuliko Mungu na amri zake. Hili ndilo kosa lililotendeka ndugu zangu na mwishowe walishindwa kuona mengi-walishindwa kumjua Mungu, kutambua amri zake, na hata kushindwa kumpokea Masiha. Hiyo ndiyo iliyokuwa hasara yao.

Nasi ndugu zangu tumshukuru Mungu kwa kukubali kukaa kanisani kwetu katika Ekaristi na sisi hata kuja kusali hapa. Hili ni tendo la upendo toka kwa Mungu, angeweza kukataa lakini kakubali mwenyewe kufanya kitu kama hiki. Hivyo, tuheshimu kanisa na kuheshimu Ekaristi. Kadiri tutakavyoiheshimu, ndivyo hivyo na Mungu atakavyoendelea kutubariki na kukaa kati yetu na kutuletea baraka zake. Tukikosa heshima kwa sakramenti zetu tutajiletea laana wenyewe kwa kujifungia baraka. Tuchote baraka kwa heshima kuu.

Maoni


Ingia utoe maoni