Jumamosi, Februari 08, 2020
Tafakari ya kila siku
Jumamosi, Februari 8, 2020,
Juma la 4 la Mwaka wa Kanisa
Mk 6: 30-34.
YESU MWENYE HURUMA!
Yesu ni kiongozi bora mwenye huruma kwa wanyonge katika jamii, mwenye huruma pia kuelekea mahitaji ya binadamu. Baada ya Wanafunzi kurudi kutoka utume kuhubiri, Yesu anapendekeza wapumzike. Lakini yeye mwenyewe, akiacha mahitaji yake kama kupumzika, chakula, nk, alianza kuwahudumia watu, kwa sababu walikuwa na uhitaji mkubwa zaidi. Binadamu kwa kawaida tena mara nying anajifikiria yeye kwanza,( binafsi); na anatimiza mahitaji yake kwanza. Lakini Yesu ni mfano halisi wa kutokuwa na ubinafsi.
Jibu la Yesu linaonesha moyo wenye huruma. Anasukumwa na huruma kwa ajili yao na anaendelea kuwafundisha mambo mengi. Haya yanatokea kwasababu ya sababu nyingi. Kwanza, kwa sababu ya hamu kubwa ya ndani ya watu kuhusu yeye. Walivutwa kwa Yesu, kumsikiliza na kujifunza kwake. Pili, ni kwasababu Yesu alikuwa na hamu kubwa ya kuwa na watu wake. Alitamani kushirikisha moyo wake na wao na kuwachunga kama mchungaji, kuwaongoza kwenye ukweli aliokuja kuufunua. Yesu alikuwa Mchungaji wa kweli aliye wapenda kondoo wake na kuwakaribisha daima.
Inapaswa iwe hivi pia kwetu sisi. Tunapaswa tutafute daima kuwa naye, kumpenda na kufuata amri zake. Tunapaswa kujitoa bila kuchoka kumtafuta bila kujali ni ugumu ghani tuna upata. Tuna jukumu, kwa upendo tumtafute na kumpata Bwana wetu. Na Yesu, atafanya jukumu lake la kutuchunga na kutuongoza kama mchungaji na kutufundisha mambo mengi. Ataruhusu moyo wake uongozwe na huruma juu yetu na kutuvuta karibu naye.
Kuna msichana mmoja, alikuwa anarudi kutoka shuleni, kwa miguu akiwa pamoja na wadogo zake wawili wakiume. Ghafla theluji ikaanguka ya kutisha. Wakaona kifo kipo mbele yao. Yule Msichana akatoa zile nguo zake mwenyewe za kuzuia baridi akawafunika kaka zake ndani ya nguo zile akawakumbatia, kuwalinda, kama vile alivyoweza, na mwili wake mwenyewe. Badaaye, wazazi wakatoka kwenda kuwatafuta watoto,wakawakuta wale wavulana hai na dada yao amekufa. Wenyeji wa kijiji kile wakajenga mnara wa kumbukumbu pale, wakaandika "Msukumo kwaajili ya kulinda uhai". Je! Imani yako kwa Yesu inakuongoza ufanye nini ? Leo Yesu anatukaribisha na kutuongoza tumuige yeye, je upo tayari?
Sala:
Bwana, nakupenda wewe na ninatoa maisha yangu kwako. Ninakuomba unijaze daima na na moto wa kutaka kukutafuta kila siku. Ninakushukuru kwa huruma yako na uchungaji wa roho yangu. Ninaomba nijipumzishe karibu na moyo wako daima. Yesu nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni