Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Januari 24, 2020

Januari 24, 2020
JUMA LA 2 LA MWAKA

1Sam. 24:2-20
Zab. 57:1-3, 5 (K) 1
Mk 3: 13-19

KUELEKEA MLIMANI!

Leo Yesu anawaita wale aliotaka kujenga nao jumuiya moja. Yeye aliwateua kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye na kwamba apate kuwatuma kuhubiri na kuwapa mamlaka ya kuwafukuza pepo. Yeye anawakaribisha katika uhusiano maalum na yeye mwenyewe ili aweze kuwatuma,na walete mabadiliko katika dunia hii.

Kitu kimoja muhimu ni kwamba Yesu yupo na wanafunzi wake “mlimani”. Jambo hili linaonesha au kutoa funzo/alama muhimu. Uwepo wa mitume kuhubiri na kutoa pepo unaanza tu mara baada ya Yesu kwenda mlimani nao. Kwanini anafanya hivyo mara baada tu ya kuwaita mlimani?

Mlima ni alama ya safari yetu kumwelekea Mungu. Ni alama kwamba tunapaswa kupanda kumwelekea Yeye. Na inaonyesha kwamba tunaweza kwenda kufanya mapenzi ya Mungu tu pale ambapo tumeshaenda kumuona na kukutana nae. “Mlima” tunaoitwa kuupanda ni “sala”. Tunapaswa kupanda mlima kila siku kwenda kukutana na Bwana, kumtafuta katika maisha yetu kwa maisha ya ndani na kujikabidhi kwake. Yesu anatuita sisi kwake pale ambapo yupo anatusubiri ili tuweze kuwa naye tukifurahi uwepo wa utukufu wake. Tusipo enda kukutana na Yesu katika mlima, itakuwa vigumu kutimiza utume wake mtakatifu. Tutakuwa tumepungukiwa katika kuleta huruma na mapendo ulimwenguni. Yesu anakupa nafasi ya kumfuata katika mlima wa sala. Mjibu mwaliko wake ili aweze kukutuma kutimiza amri yake ya mapendo.

Sala:
Bwana, ninakubali mwaliko wako wa upole wa kwenda mlima wa Imani na sala. Natamani kukutafuta na kuwa nawe. Ninapo kutana nawe katika sala, nipe neema ninazo hitaji ili niweze kwenda ulimwenguni kutimiza mapenzi yako. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni