Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Novemba 23, 2019

Jumamosi, Novemba 23, 2019
Juma la 33 la Mwaka

Jumamosi, kumbukumbu ya Bikira Maria.

1Mak 6: 1-3;
Zab 9: 1-3, 5, 15, 18 (K) 15;
Lk 20: 27-40.


MUNGU WA WALIO HAI

Masadukayo walienda kwa Yesu kwenda kumtega kwa kumpa mfano mgumu ili waweze kumkamata kwa maneno yake. Wanamueleza habari ya ndugu saba walio oa mke mmoja kwa nyakati tofauti tofauti na wote wakafa bila kupata mtoto. Baada ya mmoja kufa mwingine alimchukua mke wa ndugu yake, na wote saba walikufa bila kuwa na mtoto. Na sasa wanamuuliza Yesu “Katika ufufuko wa wafu huyo mke atakuwa mke wa nani?” Walimuuliza Yesu swali hili ili kumtega kwani Masadukayo wenyewe hawakuamini kuhusu ufufuko wa wafu. Yesu anawapa jibu akiwaambia kwamba ndoa ni kwa ajili ya wana wa ulimwengu huu na sio kwa wana wa ufufuko. Jibu la Yesu liliwamaliza na kulegeza mtego wao juu ya Yesu, na Waandishi walifurahi kwani Yesu alionesha kwamba kuna ufufuko wa wafu kwani wao huamini.

Ingawaje vile vitabu vitano vya Musa havina sehemu iliyo andikwa moja kwa moja kuhusu ufufuko, Masadukayo walikataa kukubali ufufuko kwani wao wana amini tu vitabu hivi vitano-Torah. Yesu mwenyewe anaamua kutumia kitabu kimoja wapo kuonesha ufufuko. Na anatumia kitabu cha Kutoka 3:6 ambapo Mungu anasema, ‘mimi ni Mungu wa Abraham…: Mungu hasemi “nilikuwa Mungu wa Abrahamu” bali anasema kwamba “mimi ni Mungu wa Abraham…”. Ambapo ni wakati uliopo. Hii ina maana kwamba Abraham, Isaka na Yakobo wapo hai na hawajafa, bali walizaliwa kwa ufufuko katika maisha mengine. Kukubali ufufuko inakuja baada ya kukutana na Kristo. Kukutana na Yesu kunamsadia mmoja kuwa huru kutoka katika dhambi, nje na ndani mwetu. Ufufuko ni jibu la mwisho la Mungu juu ya kifo.

Kitu kimoja ambacho ujumbe huu wa Injili unatuletea ni kwamba ukweli ni mkamilifu na hauwezi kupindishwa. Daima ukweli unashinda hata kama kwa kuchelewa! Yesu kwakusema kwamba ni kweli kulifunua pazia lililokuwa mbele ya macho ya Masadukayo. Anaonesha kwamba hakuna ujanja wa mwanadamu unaweza kuficha ukweli wenyewe. Ukweli wa Injili unatuambia kwamba haijalishi tumechanganyikiwa namna gani, ukweli upo. Haijalishi ni kipi tumeshindwa kuelewa tukitafuta ukweli tutaupata.

Tafakari, leo ni kitu gani kinacho kupa changamoto sana au ni swali gani ngumu sana katika safari yako ya Imani. Pengine ni kuhusu maisha baada ya maisha haya, au pengine ni kuhusu mateso, au uumbaji. Pengine ni kitu binafsi cha ndani. Au pengine haujakaa chini ukaja na swali kwa ajili ya Bwana wetu. Haijalishi ni kipi, kutafuta ukweli katika yote na kumuuliza Bwana wetu hekima ili uweze kuingia kwa ndani kabisa kuhusu Injili.

Sala:
Bwana, ninatamani kufahamu yote ambayo umetufunulia. Ninatamani kufahamu mambo yote ambayo yananichanganya na kuleta changamoto katika maisha yangu. Nisaidie kila siku ili niweze kuzamisha Imani yangu kwako na uelewa wangu juu ya ukweli wako. Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni