Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Novemba 14, 2019

Alhamisi, Novemba 14, 2019.
Juma la 32 la Mwaka


Hek 7: 22 – 8: 1;
Zab 119: 89-91, 130, 135, 175 (K) 89;
Lk 17: 20-25.


UFALME WA MUNGU KATI YETU!

Mtoto mdogo wa miaka minne alimuuliza babu yake ambaye alikuwa amesimama karibu na kisima cha maji. Mtoto huyu akamuuliza babu yake, “Hivi Mungu anaishi wapi”? Yule babu akamnyanyua yule mtoto juu ya kisima akamwambia tazama ndani unaona nini kwenye maji, baada ya kuona kivuli chake ndani ya maji yule mtoto akasema najiona mwenyewe. Ahaa yule babu akajibu! Basi Mungu anaishi ndani yako. Ni katika moyo wa mwanadamu wenye upendo ambao Mungu hukaa.

Ufalme wa Mungu upo kati yenu! Ina maana ghani? Ufalme wa Mungu upo wapi na unakuwaje katikati yetu? Ufalme wa Mungu unaweza kuzungumziwa katika hali mbili. Siku ya mwisho atakapokuja Kristo, ufalme wake utakuwa wazi kwa kila mtu. Ataondoa dhambi zote na maovu yote na yote yatafanywa upya. Atatawala milele na ukarimu utalinda kila moyo na akili. Lakini pia Ufalme wa Mungu upo pia kati yetu. Ni ufalme ambao upo kwa neema unaoishi ndani ya mioyo yetu kwa njia isiyo hesabika kila wakati.

Kwanza kabisa Yesu anatamani kuwa ndani ya mioyo yetu na kuongoza maisha yetu. Swali la muhimu ni hili, “Je, nina mruhusu yeye atawale maisha yangu?” Yeye sio mfalme anayetawala kwa mabavu. Anatuita sisi tumpe ufalme wa maisha yetu. Anatualika sisi aweze kuwa mhusika mkuu wa maisha yetu. Kama tutamrushusu yeye atatuwekea sheria ya mapendo ndani mwetu. Sheria hii itatuburudisha na kutufanya upya. Pili, uwepo wa Yesu upo kati yetu. Ufalme wake upo kila mahali na muda wowote tunaopenda na kila mahali ukarimu upo. Kila mahali ufalme upo na neema ipo kazini. Mungu yupo katika hali nyingi katika maisha yetu. Tunapaswa tutambue hilo na kuvutwa na hali hii na kuipenda. Haijalishi Mungu yupo mbali kiasi ghani tunavyoweza kufikiria, haijalishi ni matatizo mangapi yapo katika maisha yetu na mizigo mingapi, anataka tusiwe na shaka. Ufalme wa Mungu, ni Mungu mwenyewe yupo kati yetu. Amini hilo na maisha yatachukua mtazamo mpya na matumaini mapya.

Tafakari leo, juu ya uwepo wa Mungu kati yetu. Je, unaona hilo ndani yetu? Je unauona ndani yako? Je, unamualika Yesu kuongoza maisha yako? Je, unamkiri yeye kama Bwana wako? Je, unamuona yeye akija kwako katika hali mbali mbali au kwa wengine na katika hali yako mwenyewe? Mtafute yeye kila wakati naye ataleta furaha ndani ya moyo wako.

Sala:
Bwana, ninakualika wewe, njoo utawale ndani ya moyo wangu. Ninakupa moyo wangu uulinde. Wewe ni Bwana wangu na mfalme wangu. Ninakupenda wewe na ninatamani kuishi kadiri ya mapenzi yako matakatifu. Yesu nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni