Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Oktoba 30, 2016

Jumapili, Oktoba 30, 2016.
Dominika ya 31 ya Mwaka C wa Kanisa

Hek 11:22-12:2;
Zab 144: 1-2, 8-11, 13-14;
2The 1:11-2:2;
LK 19:1-10.


MUNGU HUJAZA UTUPU WETU!

Mt. Augustino alisema “Mioyo yetu imeumbwa kwa ajili yako Ee Bwana, na haitatulia mpaka itakapotulia kwako”. Mwana mahesabu na Mwana sayanzi mmoja wa Ufaransa Blaise Paskali aliandika “Kuna sehemu ya wazi ndani ya mioyo yetu kwa ajili ya Mungu ambayo ni Mungu pekee aweza kuijaza”. Aliamini kwamba bila Mungu, maisha hayaja kamilika. Mcheza Tenesi Maarufu Boris Becker alikiri hili pia. Becker huyu alijaribu kujiua kwasababu ya kupoteza matumaini na kujisikia utupu. Ingawaje alikuwa maarufu na aliyefanikiwa, kuna kitu kilikasoro katika maisha yake. Alisema “ Nimeshinda mashindano mara mbili, kama mchezaji mdogo. Nilikuwa na mali zote na yote nilio hitaji: fedha, magari, kila kitu.” Alikuwa na kila kitu lakini hakuwa na furaha. Ndani ya moyo wa kila mwanadamu ulimwenguni kuna sehemu ya wazi ambayo ni Mungu pekee anaweza kuijaza. “Mamilionea mara nyingi ni watu walio wapweke na hata wasanii mara nyingi hawana raha walionayo mashabiki wake” alisema O. Sanders

Injili ya leo inamwongelea mtoza ushuru Zakayo. Alikuwa mtu tajiri na alikuwa ameshajifanyia fedha nyingi. Lakini alichukiwa na watu wengine, sio kwamba aliwatoza tu ushuru zaidi, lakini kwasababu alikuwa anawasaidia Wapagani wa Kirumi ili kuwakandamiza watu wa nchi yake mwenyewe. Alichukuliwa kama mdhambi wa hadharani, aliyetengwa na asiye safi mbele za Mungu. Mmoja anaweza kuona hilo, japo alikuwa mtu mwenye fedha na kupenda kufanya lolote apendalo, huyu mtoza ushuru aliishi maisha ya upweke, alitengwa na watu wake mwenyewe na alijitenga kutoka kwa Mungu na alikosa kitu flani katika maisha yake.

Zakayo alisikia mambo mengi kuhusu Yesu na alitamani kumuona . Lakini kwasababu alikuwa mfupi alizuiwa na umati. Aliwaza njia ya kumuona Yesu bila kutambuliwa na mtu yeyote. Alipanda juu ya mti huku akijificha ili amwone Yesu. Yesu alitambua Zakayo yupo juu ya mti na anamwambia “Zakayo, shuka upesi, kwani leo nitakuwa katika nyumba yako” (Lk 19:5). Badala ya kumuhukumu Zakayo Yesu anamuonesha upendo. Yesu ni mchungaji Mwema kweli, anaye warudisha waliopotea na kuwarudisha zizini.

Inamaanisha pia Yesu anawapenda wote tunaowachukia na kuwaona kama wadhambi wa mwisho, na ni yeye pekee anayeweza kuhukumu mienendo yao na mioyo yao ya ndani. Hali hii ya Yesu mara nyingi imewarudisha watu na kuwafanya watubu na kusamehewa. Hata kama watu wanafanya mabaya, tunapaswa kuwajali na kuwapenda na kujaribu kuona ni kitu ghani kinacho sababisha matatizo hayo ndani mwao. Pia wakiwa mezani Yesu haku mhubiria Zakayo kwamba anapaswa kutubu au kwamba ataenda motoni. Yesu lakini anawapokea wadhambi. Zakayo aliongea zaidi na moyo wake na anasema maneno mazuri kabisa. Zakayo ana simama na anamwambia Bwana wazi wazi mbele ya watu wtoe. “ Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.”. Kwa kutoa nusu ya mali yake na kuwapa maskini, na bado kuwalipa wale alio wachukulia kwa hila, ni hakika utajiri wa Zakayo utakuwa umeisha au anabakiwa na kidogo sana. Je, ni nani anahitaji fedha nyingi namna hiyo wakati umeshapata maana halisi ya maisha?

Katika somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Hekima linaongelea umuhimu wetu mdogo sana ukilinganisha na Ulimwengu mzima. Tupo kama puche ya nafaka, au tone la umande, lakini pamoja na umuhimu wetu mdogo kabisa ukilinganisha na vitu vingine, sisi tunapendwa na Mungu sana. Mungu aliviumba vitu vyote na anavipenda alivyoviumba. Kama Mungu hakufikiria kuhusu sisi, tusingekuwepo, kwa hiyo tunafahamu anatufikiria sisi, na hata tunapo mkosea, kumsahau, yeye hatusahau sisi kamwe na hachoki kutusamehe. Unaweza kuona ukuu wa Mungu hapa, tofauti kabisa na Mwanadamu, waweza kufikiria mtu anakukosea mara nyingi na unamsamehe tu, tuseme mfano hata mara tatu tu, na pengine kosa lile lile, sijui waonaje? Wengine tungeweza hata kutafuta mbinu za kuhama sehemu husika ili tusimwone aliyetukosea au kufanya kitu kingine. Mungu ni Baba mkamilifu- anatafuta njia ya kutuonesha tunakosea au tuna msahau, na kwa njia hiyo tunarudi kwake tena. Yeye ni Baba mkamilifu, ni Mchungaji mwema.

Mt. Paulo anatuambia tujaribu kila wakati kuwa waaminifu ili tustahili upendo mkubwa wa Mungu, tukitazama mbele ili kujiunga naye. Kama Zakayo anatuita sisi kwa majina yetu, na anatuambia tumwalike nyumbani kwetu, katika maisha yetu. Jibu la Zakayo ni kwamba, “Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.” Jibu letu kwa Yesu ni lipi? Na tuna mwahidi nini leo? Je, upo tayari kushuka huko kwenye mti umkaribishe Yesu nyumbani mwako?

Kuna pia Zakayo wengi (wake na waume) waliojificha juu ya mti ambao sisi hupita chini yake kila siku. Wanaweza kuwa maskini, waliotengwa, wagonjwa, na watu walio na matatizo mengi tunaokutana nao. Yesu anatupa changamoto ya sisi kutazama juu na kuwakaribisha kwenye chakula chetu. Katika mwezi huu wa mwisho wa mwaka wa huruma ya Mungu, Yesu anatukumbusha tena kuhusu matendo ya huruma. Tunaalikwa kufanya kitu, kwa kuwakaribisha watu hawa kwa upendo usio na masharti. Tutashangazwa tunaweza kueneza habari njema zaidi kwa kugusa mioyo ya watu zaidi kuliko kuhubiri kwa nguvu kubwa kabisa kwa maneno tu.

Sala: Bwana Yesu, naomba nijaze utupu wa moyo wangu na wewe. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni