Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Septemba 18, 2019

Tafakari ya kila siku
Jumatano, Septemba 18, 2019,


1 Tim 3: 14-16
Zab. 111: 1-6
Lk. 7:31-35

Kanisa kama familia moja kubwa

Wabatizwa wote ni watoto wa jumuiya au familia ya Mungu na nyumba ya Mungu. Mt. Paulo ananukuu kanuni ya Imani iliyokuwa maarufu kati ya waamini; “alidhihirishwa katika mwili, akajulikana na kuwa na haki katika roho”. Injili takatifu inarejea hekima ipatikanayo katika kitabu cha mithali iliyotumika katika maagizo ya mzazi kwa mtoto au Rabbi(mwalimu) kwa mwanafunzi wake. Wasomi wa Biblia wanawea bayana kuwa huenda Mt. Paulo hakutunga wimbo huu bali alinukuu wimbo kutoka katika maandishi ya kanisa la awali.
Katika familia kila mwanafamilia huheshimika kutokana na upekee wake na talanta zake. Mt. Paulo analiona kanisa likiwa lina talanta mbalimbali, akini anasema kuwa yadumu mambo matatu:Imani, matumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita yote ni upendo. Upendo huwafanya viongozi kutokuwa watawala au wenye kujali vyeo vyao bali watu wenye kujali familia ya Mungu yaani kanisa. Kama umoja utakuwa na nguvu, itakuwa kwasababu ya kazi ya viongozi waliounganisha watu wenye Imani moja.
Kucheza kulingana na mdundo wa Bwana
Kuna taswira mbili muhimu zinazoelezea namna watu walivyoshindwa kuitikia wito wa missioni ya Yesu na ya Yohane mbatizaji. Watu hawa wamefananishwa na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza wala hamkulia. Yesu anajifananisha na watoto wapigao filimbi na anamfananisha Yohane na muombolezaji. Inaweza kuwa vigumu kuona ukweli huu kuwa Yesu anatupigia mdundo ili tuucheze lakini huu ndio uhalisia katika maisha yetu tukiwa kama wafuasi wake.
Wakristo ndio wachezao mdundo wa Kristo. kucheza mdundo wa mtu mwingine kunaweza kumaanisha kufuata kasumba Fulani, lakini sisi kama wafuasi wa Kristo tunatakiwa kusikiliza mdundo na muziki wa maisha yake na kujitahidi kuenenda katika mdundo huo. Tunatakiwa kuruhusu muziki aliocheza Yesu katika maisha yake yaani maisha , kifo na ufufuko kutuongoza katika maisha yetu. Tutakapomsikiliza Yesu kwa makini ndipo mahusiano yetu na Mungu yatakavyoimarika. Mama yetu Bikira Maria alikuwa msikivu sana kwa mwanawe Bwana wetu, alifuata mdundo wa muziki wa mwanawe kuliko mtu yeyote. Yeye ndiye kichocheo kwetu kadiri tunavyotaka kuishi kulingana na muziki wa Mwanawe Bwana wetu Yesu Kristo utupao uhai.

Maoni


Ingia utoe maoni